You are on page 1of 3

WAKALA WA USAJILI WA BIASHARA NA LESENI (BRELA)

HUDUMA ZA BRELA KUIMARIKA. PRESS COFERENCE 10.7.2013 Ndugu waandishi wa Habari Habari ya Asubuhi!! Tumekuja kuzungumza nanyi kuhusu namna Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), inavyoimarisha huduma kwa kuhakikisha kuwa wateja wake wanapata huduma bora, kwa wakati na kwa kutumia mikakati mbali mbali ya kisheria, kiutendaji pamoja na mbinu za kimtandao kwa kutumia njia za kielektroniki kwa ajili ya kupeleka huduma karibu na wananchi. Ndugu Waandishi; Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kwa kuzingatia dhana ya ushirikiano na Sekta Binafsi yaani PPP imeingia kwenye Mkataba wa ushirikiano na Chama Cha Wafanyabiashara na wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), ili waweze kutoa huduma saidizi za awali za usajili wa Makampuni na Majina ya Biashara katika ngazi ya Mikoa na wilaya Tanzania Bara. Kuchaguliwa kwa TCCIA kumetokana na wao kuwa na mtandao mpana wa kielektroniki unaounganisha ofisi zao wilayani takriban mikoa yote ya Tanzania bara hivyo kuifanya BRELA kuona umuhimu wa kuzitumia ofisi zao zilizoko nchi nzima. Wateja wa BRELA waliopo mikoani wanahimizwa kutumia ofisi za TCCIA na kuendelea kuwasilisha maombi yao ya huduma za Usajili kupitia ofisi za Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo (Tanzania Chamber of Commerce, Industry and Agriculture-TCCIA) mikoani ambapo taasisi hiyo hutuma maombi hayo BRELA ambako usajili hufanyika na kurejesha vyeti vya usajili TCCIA mkoani hivyo kutokulazimika kusafiri kuja Dar es Salaam kwenye Ofisi za BRELA kupatiwa huduma za usajili. Utaratibu huu wa ushirikiano baina ya BRELA na TCCIA ulianza Decemba 2012, na zaidi ya maombi 500 yamesajiliwa kupitia ofisi za TCCIA mikoani. Kupitia utaratibu huo, gharama za usajili wa Jina la Biashara ni sh. 6,000/= ambazo wateja hulipia na kupatiwa stakabadhi za BRELA na pia TCCIA inatoza kiasi kidogo cha fedha sh. 2,000/- kwa kila Jina la Biashara kwa ajili ya huduma za kiutawala ikijumuisha gharama za utumaji wa maombi hayo.

Aidha, Kwa upande wa Usajili wa Makampuni ada ya usajili inayotakiwa kulipwa itategemeana na kiasi cha mtaji Mteja anachokiandika kwenye Katiba ya Kampuni anayotarajia kuisajili. Gharama yake inaanzia sh. 50,000/= kwa mtaji wa zaidi ya Sh. 20,000/= - 500,000/= na kiwango cha ada cha juu kabisa ni sh. 300,000/= kwa mtaji ambao ni zaidi ya 30,000,000/= ambapo utapata stakabadhi ya BRELA na TCCIA watatoza gharama ndogo ya sh. 5,000/= kwa kila kampuni kwa ajili ya gharama za kiutawala ikijumuisha gharama za usafirishaji. Utaratibu huu wa ushirikiano wa kutoa huduma kati ya BRELA na TCCIA umesaidia kwa kiasi kikubwa kusogeza huduma za BRELA karibu na wananchi, hususan wa mikoani ambapo sasa hawalazimiki kuja Dar es Salaam kufuata huduma za BRELA. Hii ni hatua ya awali wakati tunaendelea kuboresha zaidi huduma mikoani ikiwa ni pamoja na kutumia mifumo ya TEHAMA. Ndugu Waandishi wa Habari, Mabibi na Mabwana; Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) hutoa baadhi ya huduma za usajili kwa njia ya mtandao, hivi sasa Majina yote ya Makampuni na Majina ya Biashara yamewekwa kwenye mtandao. Mteja akiingia kwenye tovuti ya BRELA www.brela-tz.org, anaweza kuona orodha ya Makampuni yote yaliyosajiliwa Tanzania Bara na kufanya upekuzi wa majina Online name search ili kutambua iwapo jina la biashara analolitaka kusajili limeshasajiliwa au la, kabla ya kutuma maombi ya Usajili. Aidha, fomu zote za usajili zinapatikana kwenye tovuti hiyo. Pia tumeweka katiba mfano inayojulikana kwa lugha ya kigeni kama Memorandum and Article of Association kwenye tovuti ambayo mteja anaweza kutumia bila gharama yeyote kujitengenezea katiba ya kampuni yake. BRELA ipo katika mkakati wa kuweza kutoa huduma kwa njia ya mtandao wa kielektroniki (online registration), kwa kuanza, imekwisha kuweka nyaraka za mafaili kwenye mfumo wa kieletroniki ambapo unaweza kupata jalada kwenye kompyuta. Ndugu Waandishi wa Habari, Mabibi na Mabwana; BRELA ipo mbioni kurahisisha njia za malipo kwa kutumia mabenki kwa kuanzia na CRDB na NMB. Mpango huu unatarajiwa kuanza rasmi tarehe 15.7.2013 na benki ya CRDB Mpango huu utawawezesha Wadau kulipa ada za usajili kwa njia ya benki popote walipo. Mpango wa baadaye ni kuweza kusajili na kupata huduma popote alipo kwa kutumia
2

mtandao ambao utatuwezesha kufikia kwenye ndoto yetu ya kutoa huduma bora na kwa wakati kwa kuzingatia viwango vya kisasa vya kimataifa kulingana na dira ya Wakala. BRELA ilianzishwa na kuzinduliwa rasmi tarehe 9 Desemba 1999 chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa Sheria ya Wakala za Serikali namba 30 ya mwaka 1997. Makujumu makuu ya BRELA ni kusajili Makampuni; kusajili Majina ya Biashara; Alama za Biashara na Huduma; kutoa Hataza - Uvumbuzi kwa muda maalum (patents of inventions) na Kutoa leseni za Viwanda na kusajili Viwanda. Lengo kubwa la BRELA ni kuhahikisha kuwa huduma za usajili zinapatikana pale zinapotakiwa kwa wepesi na urahisi wakati wote na popote kwa kutumia njia za kisasa. Ninawashukuru sana. Kwa niaba ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA); Taarifa hii imetolewa na Bw. Bosco Gadi, Kaimu Meneja Huduma, Utawala na Fedha, BRELA, Email; bosco.gadi @ brela-tz.org; au ringgadi@gmail.com au Simu na 0713 233 180; 2180141/113, Fax 2180371: na Bw. Andrew Mkapa, Naibu Msajili, Mkuu wa Idara ya Sheria za Biashara: andrew.mkapa@brela-tz.org au abwmkapa@hotmail.com , Simu na. 0713 335618 ; 2180141/113, Fax 2180371:

You might also like