You are on page 1of 2

Oktoba 11, 2013 Na Kaimu Balozi Virginia M.

Blaser

Kwa nini yakupasa uwe mfano kwa mtoto wa kike wa Kitanzania Pamoja na jamii mbalimbali duniani kote, Marekani ina fahari kubwa kuadhimisha tarehe 11 Oktoba kama Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike. Siku hii ilianzishwa ili kutambua haki za watoto wa kike na kuimarisha dhamira na jitihada za kimataifa za kutokomeza unyanyasaji, ubaguzi na ukatili wa kijinsia na ubaguzi wa kiuchumi unaowaathiri zaidi watoto wa kike. Ushahidi unaonyesha kuwa nchi yoyote, ikiwemo Tanzania na Marekani inaweza tu kuendelea kiuchumi, kijamii na kisiasa pale ambapo wasichana wanashiriki kikamilifu katika nyanja zote za maisha ya jamii na pale wanapolindwa dhidi ya ubaguzi na vitendo vingine vyovyote vinavyoweza kuwaathiri mathalan, ndoa za utotoni na za kulazimishwa na ukatili wa kijinsia. Siku hii inatupa fursa ya kipekee ya kutafakari jinsi gani tunaweza kufanyakazi pamoja ili kuhakikisha kuwa vijana wetu wote - wa kike na wa kiume - wana fursa sawa ya kuchangia katika jamii yao na kujenga mustakabali mwema kwa wao wenyewe, familia zao na mataifa yao. Rais Barak Obama na Waziri wa Mambo ya Nje John Kerry wamelifanya suala la kuinua hadhi ya wanawake na watoto wa kike kuwa jambo la kipaumbele la kidiplomasia la Marekani. Kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania, wabia wengine wa kimataifa na asasi mbalimbali zisizo za kiserikali, Watu wa Marekani wamekuwa wakisaidia jitihada mbalimbali za ulinzi, maendeleo na uwezeshaji wa watoto wa kike wa Tanzania ili waweze kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya nchi yao na dunia kwa ujumla. Hata hivyo, leo hii ninapenda kutoa wito kwa Watanzania wote, wake kwa waume, iwe ni baba au mama, kaka au dada, kiongozi au hata rafiki. Ninamwomba kila mmoja wenu achague mtoto mmoja wa kike katika jamii yake atakayemsaidia ili aweze kufikia upeo wa uwezo wake. Wasiliana na mtoto huyo wa kike, ongea nae na zifahamu changamoto zinazomkabili katika maisha yake ya siku hadi siku. Shirikiana naye katika kutambua vikwazo vinavyomkwamisha kisha msaidie kuvikwamua ili aweze kusonga mbele.

Nilipokuwa msichana, kinara wangu alikuwa ni mama yangu mzazi aliyenikuza na kunifanya niamini kwamba ninaweza kufikia ndoto yoyote ile. Alikuwa mfano hai wa kuvunja dhana potofu dhidi ya watoto wa kike pale alipopata shahada ya juu ya uchumi katika wakati ambapo haikuwa kawaida kwa wanawake katika majimbo ya mashambani Kusini mwa Marekani kufanya jambo hilo. Akilazimika kuingia darasani katika kipindi cha likizo ya kiangazi kwa kuwa wakati huo chuo kikuu alichokuwa akisoma hakikuruhusu wanawake kuhudhuria masomo katika muhula wa masomo wa kawaida, mama yangu alipambana na ubaguzi ili kufikia ndoto yake. Nilipokuwa kigori nilijiingiza katika shughuli ambazo kwa kawaida zimehodhiwa na wanaume -- kutoka michezo hadi taaluma -- mama yangu aliniunga mkono kwa moyo mmoja. Akinishangilia katika mbio zote nilizoshiriki na akinipa moyo na kunihimiza nijaribu tena pale niliposhindwa na kuanguka. Mwandishi mmoja wa Kimarekani aitwaye Mark Twain alipata kusema kwamba watu wenye busara, uwezo na upeo mkubwa huwafanya wengine wajione kuwa na wao wanaweza kuwa na busara, uwezo na upeo mkubwa. Hivi ndivyo mama yangu alivyonifanyia, na ndivyo ninavyomsihi kila mmoja wetu amfanyie mtoto wa kike katika jamii zetu. Pale mtoto wa kike anapoendelea, taifa zima linaendelea. Wataalamu wengi wanaoheshimika wa masuala ya uchumi (mfano Ripoti ya World Economic Forum kuhusu Tofauti za Kijinsia) wamebaini kuwa nchi ambazo zina uchumi uliostawi na wenye ushindani ni zile ambazo wanaume na wanawake wana fursa sawa katika nyanja mbalimbali za jamii ikiwa ni pamoja na elimu, afya, ushiriki katika uchumi na ushiriki katika siasa. Siku hii ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike inatupa sisi sote fursa ya kujadili masuala haya muhimu na njia zitakazotuwezesha kufanya kazi kwa pamoja kuondoa vikwazo vinavyoweza kuwakwamisha watoto na vijana wetu wa kike na wa kiume wasifikie upeo wa uwezo wao. Pamoja na kujenga ufahamu huu, kwa mara nyingine tena napenda kutoa wito kwenu nyote kuchukua hatua mahsusi katika jamii zenu. Chagua mtoto mmoja wa kike wa Kitanzania katika jamii yako na uwe mwalimu wake, msaada wake na kiongozi wake. Kwa kumsadia mtoto huyu wa kike wa Kitanzania kukabiliana na kuzishinda changamoto katika maisha yake, utakuwa unasukuma mbele gurudumu la maendeleo ya taifa lako na ya dunia. Nawe pia utakuwa kinara.
______________________________________________________________________________

Virginia M. Blaser ni Kaimu Balozi wa Marekani katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

You might also like