You are on page 1of 1

TOFAUTI KATI YA MALIPO YA LIKIZO NA MSHAHARA WA MWEZI WA KUMI NA TATU (13th Month salary)

Kumekuwa na uelewa tofauti juu ya maana ya malipo ya likizo na mshahara wa mwezi wa kumi na tatu. Mara nyingi watu wamekuwa wakidhani mshahara wa kumi na tatu (13th Month salary) ndio malipo ya likizo yanatamkwa katika Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, 2004. Lakini, tofauti na dhana hiyo, masuala haya mawili yanatofautiana. Malipo ya likizo ni nini? Kwa ilivyo kawaida, mwajiriwa hulipwa mshahara kila mwisho wa mwezi kama malipo ya kumfanyia kazi mwajiri wake kwa muda wa mwezi mzima. Lakini sheria pia inamtaka mwajiri ampatie mfanyakazi wake likizo ya angalau siku 28 ndani ya muda wa miezi 12 ya kazi. Kwa maana hiyo, sheria inampatia mwajiriwa haki ya kupumzika kwa angalau siku 28 katika kipindi cha miezi 12 ya kazi. Hii ina maana kwamba katika kipindi cha miezi 12 ya kazi, kuna mwezi mmoja ambao mwajiriwa hatamfanyia kazi mwajiri wake. Sheria pia inasisitiza kuwa, katika kipindi hicho cha siku 28 ambapo mwajiriwa atakuwa akipumzika, mwajiri anatakiwa kumlipa mwajiriwa kiasi cha fedha kinacholingana na malipo anayostahili kupata mwajiriwa huyo kama angekuwa akifanya kazi kwa siku hizo 28. Katika kutekeleza agizo hilo la shria, mara nyingi mwajiri humpatia mwajiriwa malipo yanayolingana na kiasi cha mshahara wake wa mwezi katika zile siku 28 za mapumziko. Hivyo, mshahara huo ndiyo malipo ya likizo; mwajiriwa analipwa bila kumfanyia kazi mwajiri wake. Hayo ndiyo malipo ya likizo kwa mujibu wa sheria. Mshahara wa kumi na tatu ni nini? Mshahara wa kumi na tatu ni malipo anayopewa mwajiriwa na mwajiri wake kama bakshishi kwa kumfanyia kazi kwa mwaka mzima. Malipo haya hutolewa kila mwisho wa mwaka, baada ya shughuli za mwaka mzima za mwajiri kufikia mwisho. Katika baadhi ya nchi malipo hayo yamewekwa kisheria kama sehemu ya marupurupu ambayo mwajiriwa anastahili kuyapata kila mwisho wa mwaka. Kuna maelezo kadha wa kadha kuhusu chanzo cha malipo haya lakini vyanzo vingi vinasema msingi mkubwa wa malipo haya ni kuwawezesha wafanyakazi kumudu gharama za sikukuu nyingi zinazoangukia mwishoni mwa mwaka kama vile krismas na mwaka mpya. Hapa Tanzania malipo hayo hayapo kisheria, lakini baadhi ya waajiri wamekuwa wakiwapatia waajiriwa wao kama bakshishi.

You might also like