You are on page 1of 1

MWAJIRIWA NI NANI?

Kwa muda mrefu sasa jamii imekuwa na uelewa usiyo sahihi kuhusu tafsiri ya neno mwajiriwa. Watu wamekuwa wakidhani kuwa mwajiriwa ni yule mtu tu aliye na mkataba wa kazi na mwajiri wake. Na kwamba mkataba huo lazima uwe ni wa maandishi. Lakini hebu tuangalie hapa chini sheria inasemaje kuhusu tafsiri ya mwajiriwa. Kwa mujibu wa kifungu cha 61 cha Sheria ya Taasisi za Kazi ya 2004, bila kujali mikataba au la, na iwapo haitathibitika vinginevyo, mwajiriwa atachukuliwa kuwa, a. mtu yeyote anavyofanya kazi chini ya uangalizi au maelekezo ya mtu mwingine; b. mtu yeyote ambaye masaa yake ya kazi yako chini ya uangalizi au maelekezo ya mtu mwingine; c. mtu yeyote anayefanya kazi katika shiriki, iwapo yeye ni mwanachama wa shirika hilo, d. mtu yeyote anayefanya kazi kwa mtu mwingine kwa wastani wa masaa angalau 45 kwa mwezi kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita; e. mtu yeyote ambaye ni tegemezi kiuchumi kwa mtu mwingine ambaye anafanya kazi au anatoa huduma kwake; f. mtu yeyote anayepewa vifaa vya biashara au dhana za kazi na mtu mwingine; au g. mtu yeyote anayefanya kazi au kutoa huduma kwa mtu moja tu. Hivyo, japokuwa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya 2004, kwa mujibu wa kifungu cha 14 (1) na 15 (1) na (2), inasisitiza mfanyakazi kupatiwa mkataba wa maandishi au kuwekewa katika maandishi makubaliano ya kazi yaliyofikiwa kwa mdomo, kutokuwepo kwa mkataba huo wa maandishi au kukosekana kwa maandishi ya kushuhudia makubaliano ya mdomo hakuwezi kumfanya mtu asitambuliwe kama mwajiriwa. Iwapo mtu aliye katika mazingira yaliyotajwa katika kifungu cha 61 cha Sheria ya Taasisi za Kazi ya 2004 ataweza kuyathibitisha hivyo mbele ya vyombo vya maamuzi na upande wa pili ukashindwa kuthibitisha vinginevyo, basi mtu huyo atachukuliwa kuwa mwajiriwa na atakuwa anastahili kupata haki zote anazostahili kupata mwajiriwa. Msisitizo wa kifungu cha 61 cha Sheria ya Taasisi za Kazi ya 2004 ulionyeshwa na Mahakama Kuu Divisheni Kazi katika Ombi la Marejeo Na. 291 la mwaka 2009 baina ya Director Usafirishaji Afrina na Hamisi Mwakabala na wenzake 25.1

Kwa marejeo zaidi na kutaka kuelewa vizuri kilichosemwa na Mahakama Kuu Divisheni Kazi katika Ombi la Marejeo Na. 291 la mwaka 2009 baina ya Director Usafirishaji Afrina na Hamisi Mwakabala na wenzake 25, tembelea sehemu iliyoandikwa MAAMUZI YA MAHAKAMA KATIKA MASHAURI YA AJIRA iliyopo katika blogu hii.

You might also like