You are on page 1of 1

HAKI YA KUPATA MSHAHARA

Haki ya kupata mshahara ni moja kati ya haki anazostahili kuzipata kila Mtanzania aliyeajiriwa. Ibara ya 23(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 inasema kuwa kila mfanyakazi anastahili kulipwa mshahara unaolingana na kazi anayoifanya, uwezo wake wa kufanya kazi, kiasi na sifa za kazi anayoifanya. Ibara 23(2) inaendelea kusema kuwa mshahara huo unatakiwa kuwa ni wa haki. Haki hii pia inapatikana katika sheria mpya za kazi katika sekta binafsi, yaani Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazi ya 2004 pamoja na Sheria ya Taasisi za Kazi ya 2004. Sheria hizi mbili zina vifungu ambavyo vinampatia mfanyakazi, aliye katika sekta binafsi, haki ya kupata mshahara. Mathalan, kifungu cha 26 cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini kinatoa ufafanuzi wa jinsi ya kukokotoa mshahara wa kima cha chini, kifungu cha 27 cha sheria hiyo hiyo kinaeleza utaratibu wa kufuatwa na mwajiri wakati wa kumlipa mfanyakazi wake mshahara ilhali kifungu cha 28 cha sheria hiyo kinaelezea utaratibu utakao fuatwa na mwajiri wakati anataka kufanya makato katika mshahara wa mfanyakazi wake. Vile vile, vifungu vya 36(1) (a) na 37 vya Sheria ya Taasisi za Kazi ya 2004, vikisomwa kwa pamoja, vinampatia waziri anayehusika na masuala ya kazi jukumu la kupanga kiwango cha kima cha chini cha mshahara anaostahili kupata kila mfanyakazi aliyeajiriwa katika sekta binafsi. Katika kulitekeleza jukumu hilo, mpaka sasa, tangu kuanza kutumika kwa Sheria ya Taasisi za Kazi ya 2004 Desemba 2006, mawaziri wanaohusika na masuala ya kazi katika nyakati tofauti wameshatoa matamko matatu ya kima cha chini cha mishahara ya wafanyakazi katika sekta binafsi. Tamko la kwanza lilitolewa Oktoba mwaka 2007, la pili lilitolewa Aprili 2010 na la tatu lilitolewa Juni 2013. Hivyo, kima cha chini cha mishahara ya wafanyakazi katika sekta binafsi kwa sasa ni kile kilichotajwa katika Tamko la Mishahara la Juni 2013.1

Kwa marejeo zaidi na kutaka kuelewa vizuri viwango vya mishahara vilivyowekwa katika Tamko la Aprili 2010 na Juni 2013, tembelea sehemu iliyoandikwa SHERIA, KANUNI, MIONGOZO YA MASUALA YA KAZI iliyopo katika blogu hii.
1

You might also like