You are on page 1of 4

TUME YA UCHAGUZI IKIAMINIKA ,MATOKEO YA UCHAGUZI YATAKUBALIKA.

Viongozi na wajumbe wa tume hii kuteuliwa na Rais moja kwa moja kunafanya wengine wasiwe na
imani katika uhuru wa utendaji wa watu hawa.Rais wa sasa ambaye ndiye huteua viongozi na
wajumbe hawa wa tume ni mwenyekiti wa chama tawala na isitoshe mara nyingine hukuta Rais
anateua wakati bado naye atakuwa mmoja wa wagombea katika chaguzi zifuatazo.

Tangu Tulipoingia katika Mfumo wa vyama vyingi mwaka 1992 na kuwa na uchaguzi wa kwanza
uliohusisha vyama vingi mwaka 1995,suala la Tume ya uchaguzi kulalamikiwa limekuwa dhahiri sana.Ni
ukweli usiopingika kuwa taasisi nyingi za nchi yetu ziliundwa katika mfumo wa chama kimoja hivyo
mtazamo wa walioanzisha taasisi hizo uliegemea katika chama kimoja.
Baada ya mabadiliko ya mfumo wetu wa demokrasia kuingia katika vyama vingi,taasisi nyingi aidha
zimeendelea kutumia mfumo wake wa zamani ama wamefanyika mabadiliko madogo sana ambayo
bado hayawezi kuleta imani thabiti kwa watu wale walio na mtazamo wa tofauti na chama tawala.Suala
kubwa kwa sasa katika chaguzi zote nchini kwetu kuanzia zile za udiwani,ubunge hadi Urais ni uaminifu
na uwezo wa tume katika kusimamia chaguzi na kutangaza matokeo halali katika chaguzi hizo.
Siku ya Tarehe 3 November 2010 majira ya saa kumi jioni,kituo cha radio cha TBC kilitangaza tamko la
mmoja wa wagombea urais kupitia chama cha demokrasia na Maendeleo(Dr.Wilbroad Slaa) akiitaka
tume ya Taifa ya uchaguzi kusitisha zoezi la kuhesabu kura mara moja.Sababu kubwa aliyoeleza ilikuwa
ni kutuhumu kuhujumiwa kura zake kunakofanywa na CCM kwa kutumia idara ya usalama wa Taifa.
Hata mara baada ya matokeo,Dr.Slaa alieleza msimamo wake wa kutoyakubali matokeo na
kutomtambua Rais Jakaya Kikwete na kususia sherehe za kuapishwa kwake ikiwa ni kuonyesha kwa
vitendo msimamo wake huo.Alieleza sababu zingine kadhaa ikiwemo usiri mkubwa katika kutangaza
matokeo kutoka vituoni,lakini pia hadi wakati mshindi anatangazwa matokeo ya maeneo yote yalikuwa
bado hayajawekwa wazi,bali yalisema ya jumla tu.Hili nalo liliongeza walakini kwa wagombea katika
uchaguzi huu.
Naye mwenyekiti wa chama cha Wananchi CUF akihojiwa na shirika la utangazaji la Amerika(VOA)
alieleza kikwazo kikubwa katika kuwa na uchaguzi huru na wa haki katika nchi ya Tanzania ni namna ya
tume yetu inavyofanya kazi.
Katika uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2010 tukishuhudia vurugu zikitokea katika maeneo mbalimbali
na nyingi za vurugu hizo zikisababishwa umwagaji wa damu.Maeneo kama ya Mwanza,Iringa,Songea na
Arusha kukiwa na matukio kadhaa yaliyosababisha kujeruhiwa au kuharibiwa kwa mali mbalimbali.
Maeneo haya yote ukifuatilia kiiini cha vurugu hizi zimekuwa ni wananchi kukosa imani na utendaji kazi
wa tume ya uchaguzi kuanzia kuhesabu kura hadi kutangazwa kwa kura hizo.Wananchi wengi huamini
kuwa tume ya uchaguzi hufanya kazi kwa niaba ya chama tawala na si vinginevyo.Matokeo
yanapochelewa tu,hisia huanza kujengwa kuwa kuna wizi unapangwa kufanyika kuwadhulumu
wapinzani.
Sababu za kutokuwa na imani na tume ya uchaguzi,ikiambatana na malalamiko ya watu kutoona majina
yao katika daftari la kupiga kura ni moja ya sababu ya watu kukosa motisha ya kujitokeza kwa wingi
katika upigaji wa kura,kwani wengi huamini kuwa kura yao inaweza isilete tofauti yoyote ile.Wengi
huamini mshindi ameshapangwa na kuchaguliwa na Tume ya uchaguzi tayari.
Mwaka 2005 Rais Kikwete alichaguliwa na wapiga kura zaidi ya Milioni 9, kiasi cha asilimia zaidi ya 80 ya
wapiga kura wapatao zaidi ya milioni 11;Mwaka 2010 Rais Kikwete akachaguliwa na wapiga kura
takribani Milioni 5 hivi, sawa na asilimia 61 na ushee ya wapiga kura wanaozidi kidogo milioni
nane.Ukweli ni kwamba idadi ya watu nchini inaongezeka(Population) lakini cha kushangaza idadi ya
wapiga kura inashuka tena kwa kasi sana.Badiliko hili la Rais aliyeshinda uchaguzi ni sawa na kushuka
kwa asilimia 20 kulinganisha na ule ushindi wa mwaka 2005.
Kwa sasa nchi yetu inakadiriwa kuwa na idadi ya vijana chini ya umri wa miaka 35 karibu asilimia 78 ya
watu wote ambao ni sawa na kusema karibu watu milioni 35 ni vijana,hii ni idadi kubwa kuliko idadi ya
watu nchini Tanzania ya mwaka 2003.Katika Taifa lenye vijana wengi hivi,kupata idadi ya wapiga kura
milioni 8 miaka 3 iliyopita ni jambo la kushtua sana.
Katika Taifa la watu la watu milioni 45 Rais kuchaguliwa na watu milioni 5,ni jambo la hatari kwa
anayechaguliwa na atakaowateua pia kumsaidia kuongoza.Kuchaguliwa na watu wachache kunatoa
ugumu wa kuongoza,ni rahisi pia kuamsha uasi.Katika mazingira haya ni kusema kisiasa kuna kundi kundi
linalokuwa halijamchagua kiongozi kuliko lile lililomachagua kiongozi huyo,hivyo kile kinachoaminiwa na
kufanywa na wasiomchagua kitawazidi wale waliomchagua na kumuunga mkono kwa sababu ya tofauti
ya idadi.
Kwa Nini Tume Ya Uchaguzi Haiaminiki?
Tume haiwezi kauminika hadi muundo wake utakapobadilika.Kwa sasa si suala la nani anaongoza tume
au nani ni wajumbe wa tume,kwa sasa swala la msingi huyo anayeongoza tume au hao walio wajumbe
wa Tume wanapatikanaje?
Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) kwa sasa huwa inaongozwa na Mwenyekiti,makamu mwenyekiti na
mkurugenzi wa tume,pamoja na wajumbe saba ambao wote huteuliwa na Rais.Akitoa maoni yake kwa
tume ya kukusanya maoni ya katiba,mwenyekiti wa Tume Jaji mstaafu Damiani Lubuva alikiri kuwa
kumekuwa na malamiko mengi hasa katika uhuru wa Tume na akapendendekeza hata kubadilishwa kwa
jina la tume na kuitwa tume huru ya uchaguzi kama ilivyo Kenya,Afrika Kusini na Ghana.
Kubadilisha jina ni sawa ila nadhani itakuwa ni sawa na kubadilisha nguo,haibadili tabia ya mtu hata
kidogo.Tunahitaji uhuru wa tume yetu utokane na imani ya watendaji wa tume hiyo kuwajibika katika
kutenda haki na sio kuonekana kuwatumikia chama Fulani.
Viongozi na wajumbe wa tume hii kuteuliwa na Rais moja kwa moja kunafanya wengine wasiwe na
imani katika uhuru wa utendaji wa watu hawa.Rais wa sasa ambaye ndiye huteua viongozi na wajumbe
hawa wa tume ni mwenyekiti wa chama tawala na isitoshe mara nyingine hukuta Rais anateua wakati
bado naye atakuwa mmoja wa wagombea katika chaguzi zifuatazo.
Tufanye Nini Kama Taifa Kujenga Imani Ya Tume?
Yako mengi yanapaswa kuzingatiwa katika kuboresha kuaminika kwa tume kwa wadau mbalimbali
katika kusimamia na kutekeleza majukumu yake nyakati za uchaguzi.
Moja uteuzi wa viongozi wa juu wa Tume lazima uwe wa uwazi kabisa na mamlaka ya uteuzi huo isiwe
kwa Rais peke yake ihusishe vyombo vingine Pia.Watu wanaoongoza tume ni lazima wawe watu
wasiotiliwa na shaka na upande wowote ule wa kisiasa(They should be proved of high level of
integrity).Ili kulithibitisha hili ni lazima uteuzi wao upitie vyombo kadhaa na uwe wazi kabisa.
Nafasi ya kuongoza tume huru ya uchaguzi na ujumbe itangazwe katika vyombo vya
habari(Magazeti,redio,televisheni) kisha watu mbalimbali wajitokeze kuomba nafasi hiyo kwa kigezo
kikubwa cha uadilifu na kutokuwa kada wa mstari wa mbele wa chama chochote cha siasa.
Baada ya hapo usahili(interview) ya walioomba wote lazima ufanyike kwa uwazi(public interview)
itakayomruhusu kila mwananchi kuangalia zoezi hilo zima.
Baada ya zoezi la usahili kukamilika majina 3 yapendekezwe kwa Rais ya watu wanaoonekana kufaa
kugombea uenyekiti na majina mengine angalau 15 ya wale ambao wanaweza kuwa makamishna wa
tume ya uchaguzi pia.Baada ya hapo,majina haya kama yalivyo watapelekwa bungeni kwa ajili ya
kusahiliwa na bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania.Kikiwa ndicho chombo kinachowakilisha
wananchi baada ya waliopendekezwa kujieleza mbele ya bunge,watachagua jina moja la Mwenyekiti na
wajumbe 7 wa tume ili kukamilisha idadi ya makamishna wa tume.Hao ndio watakuwa viongozi wa
Tume.Kwa utaratibu huu katika siasa za mfumo wa demokrasia ya uwakilishi(representative
democracy),majina ya viongozi hawa wa tume yatakuwa yamechaguliwa na wananchi kupitia
wawakilishi wao.Hii ina maana bunge litakuwa na nguvu ya kushinikiz kuondolewa kwao watakapokiuka
maadili ya kazi yao.
Ili kuepusha interest za kisiasa majina haya yatakapofika bungeni,ni muhimu kuzingatia kile kigezo cha
kwanza ambacho nilikitaja katika kusahili majina haya,yeyote ambaye anajulikana kwa namna moja au
nyingine kuwa ni mdau wa chama Fulani hataweza kupitishwa kabisa.Kwa kufanya uteuzi wa utaratibu
huu,tume itaundwa na watu ambao wameridhiwa na kupatikana kwa uwazi kuliko ilivyo hivi sasa.
Naamini,katika mchakato wa uandikaji wa katiba mpya suala la Tume ya uchaguzi kuwa huru litapewa
kipaumbele ili kujenga demokrasia ya nchi na kudumisha amani inayotokana na Haki kutendeka.
Tume ya uchaguzi ikiaminiwa,Matokeo ya Uchaguzi yataaminiwa Pia!
Joel A. Nanauka
jnanauka@gmail.com

You might also like