You are on page 1of 5

Mheshimiwa Raisi Jakaya Kikwete anaihitaji CCM kushinda uchaguzi mkuu 2010?

Wakati Tanzania inajiandaa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na raisi

wa Jamhuri ya Muungano hapo Octoba 2010, kumekuwa na hekaheka za kampeni na siasa za

vijembe zimekuwa zikitawala hapa na pale nchini kote. Kama mtanzania mwingine,nimeona

mambo mengi mazuri yamefanyika katika miaka mitano ya awamu ya kwanza ya uongozi wa

Mheshimiwa Raisi Jakaya Kikwete. Halikadhalika kumekuwa na changamoto mbalimbali za

kiuchumi, kisiasa na kijamii zilizolikabili taifa letu pendwa, vilevile kumekuwa na tafiti

mbalimbali kupima kukubalika kwa Raisi katika utendaji wake nchini mwetu, matokeo ya tafiti

hizi yalionyesha wananchi wengi kuridhika na utendaji wa Raisi wetu. Kwa kuzingatia matokeo

hayo, ningependa kuwachalenji watanzania wenzangu kuwa “kukubalika kwa Mheshimiwa

raisi kunatokana na ufanisi wake binafsi kama kiongozi makini ama ni kwa vile anatekeleza

ilani makini ya chama cha mapinduzi kinachotawala Tanzania?.”

Mara kwa mara ninapofuatilia utendaji wa Mheshimiwa raisi, na hata ninapokuwa nikisikiliza

hotuba zake katika nyakati tofauti tofauti, ninajivunia kuwa na kiongozi makini ambaye kamwe

haumi maneno, wala kuficha kitu wakati anazungumzia masuala nyeti ya nchi yetu pendwa ya

Tanzania. Kwa uadilifu na umakini wake wakati mwingine naona kuna baadhi ya viongozi ndani

ya CCM wanamungusha kwa kundekeza vitendo vya rushwa, hapo najiuliza, kama kwa kiwango

ambacho Mheshimiwa raisi anakubalika, kwa umakini wa utendaji wake na uhodari wake wa

uongozi, je , Mheshimiwa raisi akisimama kugombea uraisi bila CCM ina maana watanzania
hatutomchagua tena kuwa raisi wetu? Ama ikiwa Mheshimiwa raisi atajiunga na chama tofauti

na CCM hatutompa kura za ndiyo ili aendelee kutuongoza?

Ndugu zangu, watanzania wenzangu,maswali haya yanalenga kuamsha fikra za kutambua

kiongozi makini alipo bila kujali sana yupo kwenye chama gani. Naamini kiongozi makini katika

Tanzania anaweza kutoka CCM, CUF, UPT-Maendeleo, NCCR,TLP, CHADEMA, SAU ama chama

kingine chochote cha siasa. Katika miaka takribani kumi na nane (18) tangu kuanza rasmi kwa

demokrasia ya vyama vingi, tumeshuhudia viongozi kutoka vyama tofauti vya siasa katika ngazi

za udiwani na ubunge ingawa nafsi ya uraisi imebaki kwa chama cha mapinduzi. Ni wazi

demokrasia hi ya vyama vingi haijakomaa sana, hali inayosababisha ugumu wa kufanya

maamuzi wakati wa uchaguzi kama wakati huu. Kuendeleo kukua na kukomaa kwa demokrasia

ya vyama vingi kunahitaji viongozi watoke vyama tofauti tofauti vya siasa kulingana na uwezo

na umakini wao wa kuongoza. Hatuna budi kuwaamini viongozi kutoka vyama vya upinzani ili

waingie bungeni wakachangie sio tu ustawi wa demokrasia bali pia maendeleo ya nchi kwa

kuisimamia serikali, kuikosoa na kuingoza kwa kupitisha miswada makini katika nyanja

mbalimbali.

Ndugu zangu, tungejuaje uwezo wa Zitto Kabwe kama wana wa Kigoma wasingemwamini na

kumpa kura za ndio kuwa mbunge wao? Tungejuwaje Dr Taarabu mbunge wa CUF kuwa ni

kiongozi makini nje ya fani ya Tiba kama wananchi wa jimbo lake wasingempa kura za ndio?

Hata huyu Dr Slaa, mbunge wa Karatu tungejuaje kuwa husoma nyaraka nyeti mara mbili mbili

kabla hajazisaini ikiwa CHADEMA hawakumpa nafasi. Vipi kuhusu Mheshimiwa Magufuri,
Mheshimiwa Ngereja na hata mzee Mizengo Pinda wa CCM, wote hawa wameaminiwa na

kupewa nafasi kwa nyakati tofauti na wengi wetu tumekubali sana ufanisi wao.

Salaam zangu kwa watanzania wenzangu ni tubadili fikra zetu tunapoelekea kuchagua viongozi

watakaoshikilia nafasi nyeti za uongozi nchini mwetu kwa miaka mitano ijayo, nionavyo baadhi

ya watu wameamua kugombea nafasi za uongozi kupitia CCM kwa kuamini kuwa kazi yao ni

kuhakikisha wanafanya fitna na hila ili wapitishwe na vikao halali vya CCM, kwa vile kupitishwa

na vikao halali vya CCM ni tiketi tosha ya kushinda uchaguzi mkuu ujao kiulaini, kwani haipingiki

uwezo na nguvu za CCM katika uchaguzi huwa sio za kitoto, CCM wanajua sana kufanya

kampeni kiasi kwamba hata kama baadhi ya wagombea wa upinzani watashindana na kivuli cha

CCM, sio ajabu kukuta kivuli kinapata kura nyingi zaidi kuliko wapinzani. Matokeo haya ni

kielelezo cha ukongwe wa CCM katika kushinda chaguzi kwa kishindo. Angalizo hapa ni kuwa,

tunapoelekea kupiga kura, tusipumbazike tu na mgombea kuwa katika chama fulani pendwa, ni

vizuri zaidi kuzingatia uwezo wa mgombea katika kusimamia ilani ya uchaguzi ya chama chake,

uwezo na nia yake ya dhati kuwaletea maendeleo wanajimbo wenzake. Itashangaza sana

kuchagua viongozi ambao hawakerwi wala kuumizwa na shida za wapiga kura wao.

Jawabu la Mheshimiwa Raisi Jakaya Kikwete anaihitaji CCM ili kushinda uchaguzi mkuu hapo

Oktoba 2010, ni wazi sio rahisi kusema ndio ama hapana, lakini nionavyo ikiwa Mheshimiwa

Raisi Kikwete akigombea nafasi ya uraisi kwa tiketi ya chama tofauti na CCM, sitoshangaa

kumwona anapoteza nafasi yake ya uraisi. Kwa mtazamo huo hapo ndipo najiuliza mara mbili

mbili, siri ya ushindi ya CCM ni nini? Kwa vile pamoja na kuongoza nchi kwa miaka zaidi ya
thelathini sasa, bado nchi inahangaika na tatizo la maji ya uhakika, achilia mbali ubora wa maji

yanayopatikana, nchi bado inahangaika kuwa na umeme wa uhakika, huduma za afya na elimu

bado sio bora hata kwenye majiji kama Mwanza,Dar es Salaam, Arusha, Mbeya na Tanga achilia

mbali huko kwenye vijiji vingine ndio sababu baadhi ya vijana wa vijijini wanaona ni bora

wakimbilie jijini Dar es Salaam wakafaidi japo kidogo mema ya nchi. Pamoja na hayo, bado CCM

inashinda kwa kishindo kwenye uchaguzi mkuu unaoendeshwa kwa Haki na Huru, hili halina

ubishi. Hivyo, Mheshimiwa Raisi akithubutu kugombea kwa chama kingine tofauti na CCM, hiyo

itakuwa imekula kwake, ni wazi hana wazo hilo kwa vile anaijua sana CCM.

Ikumbukwe, lengo la salaam hizi kwa watanzania wenzangu ni kuwachalenji ili tutafakari kwa

kina mustakabali wa nchi yetu pendwa, na tufanye maamuzi sahihi wakati tunaelekea kwenye

uchaguzi mkuu, silaha zetu mkononi katika kupiga vita rushwa na tamaa ya baadhi ya

viongozi wetu kujilimbikiza mali kwa njia zisizo rasmi ni KURA, tujitokeze kwenye kampeni

zitakapoanza, tuwasikilize wagombea, tuwaulize maswali ya msingi huku tukitegemea majibu ya

matatizo yetu kwa kadri ya mahitaji yetu. Kimsingi kipindi cha kampeni wagombea wanapopita

majimboni kuomba kura ni sawasawa na mtu anapokwenda kwenye usaili wa kazi, hivyo

kampeni hizi tuzitumie kuwauliza maswali ya mambo muhimu ili tuwapime kama wanastahili

hizo ofisi nyeti za umma na kama wana uwezo wa kututumikia vema. Kama ilivyo kwenye usaili,

usipokidhi vigezo vya kazi ni wazi wenye kazi yao hawakupi nafasi , hata kama utalia machozi ya

damu, hivyo tuwape nafasi za uongozi wagombea wetu kwa kuzingatia vigezo na mahitaji yetu.

Ikumbuke kuwa ikiwa hatutopata viongozi makini , maendeleo yatachelewa kwa miaka mingine
mitano. Kwa vile ndoto za kujiletea maendeleo yetu hakuna awezaye kuzitekeleza kama sisi

wenyewe hatuwezi kufanya maamuzi thabiti.

Mwandishi : Barnabas Mbogo,


Mwanakijiji,
Kata ya Buhongwa,
P.O.Box 6243.
Mwanza

You might also like