You are on page 1of 9

MAONI NA MAPENDEKEZO YA CHAMA CHA WANANCHI (CUF) KWA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE,

KUHUSU NAMNA BORA YA UTEKELEZAJI WA SHERIA YA MABADILIKO YA KATIBA, 2011 PAMOJA NA MAENEO AMBAYO YANAPASWA KUZINGATIWA KATIKA KUIFANYIA MAREKEBISHO ILI KUIFANYA KUWA SHERIA BORA ZAIDI YAMEWASILISHWA IKULU, DAR ES SALAAM, TAREHE 02 DESEMBA, 2011

Mheshimiwa Rais, Tunatanguliza salamu za heshima na upendo kwako na tunachukua nafasi kutoa shukrani zetu za dhati kwako kwa kupokea na kuyakubali maombi yetu ya kutaka kuonana na wewe na kubadilishana mawazo na kuwasilisha maoni na mapendekezo yetu kuhusu namna bora ya utekelezaji wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, 2011 pamoja na maeneo ambayo yanapaswa kuzingatiwa katika kuifanyia marekebisho ili kuifanya kuwa sheria bora zaidi.

Mheshimiwa Rais, Chama Cha Wananchi (CUF) kinapongeza hatua ya Serikali unayoiongoza kukubali madai ya muda mrefu ya wananchi ya kutaka nchi yetu ipate Katiba Mpya itakayolingana na kuakisi matarajio na matakwa ya Watanzania katika kipindi hiki baada ya kupata uzoefu wa kutumia Katiba iliyopo tokea Uhuru wa Tannganyika mwaka 1961 na Muungano wetu wa 1964. Ajenda ya Katiba Mpya imekuwa ni sehemu muhimu ya misimamo ya CUF tokea kuasisiwa kwake na imekuwemo katika Ilani za Uchaguzi za CUF za mwaka 1995, 2000, 2005 na hata 2010. Ajenda ya kudai Katiba Mpya na kupata Tume Huru ya Uchaguzi zilikuwa ndiyo malengo makuu ya maandamano ya amani yaliyoitishwa na CUF tarehe 27 Januari, 2001. Tunapofikia hatua ya sasa ya Rais wetu kukubaliana na madai ya wananchi,

hatuna budi kukupongeza na kukuunga mkono katika hatua zote za utekelezaji wa suala hilo muhimu katika historia ya nchi yetu.

Mheshimiwa Rais, Kama inavyojieleza hapo juu, yaliyomo kwenye waraka huu tumeyagawa katika sehemu mbili. Sehemu ya Kwanza inahusu maoni na mapendekezo yetu kuhusiana na utekelezaji wa baadhi ya vifungu vya Sheria hiyo ambayo tayari umeitia saini na imeanza kutumika jana, tarehe 1 Desemba, 2011. Sehemu ya Pili inahusu mapendekezo yetu juu ya maeneo ambayo yanapaswa kuzingatiwa katika kuifanyia marekebisho Sheria hiyo ili kuifanya iwe sheria bora zaidi, hatua inayotokana na wito uliotoa wa kuwataka wote wenye maoni na mapendekezo kama hayo wayawasilishe kwako na kwamba Serikali iko tayari kuyafanyia kazi zaidi.

MAONI KUHUSU NAMNA BORA YA UTEKELEZAJI WA SHERIA YA MABADILIKO YA KATIBA, 2011 Ni jambo linalojulikana na kila anayefuatilia maendeleo ya kisiasa Tanzania kwamba kumekuwepo na mjadala mkubwa, na wakati mwengine mkali, kuhusiana na mchakato mzima uliopelekea kuandaliwa Mswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, 2011 pamoja na kupitishwa kwake. Chama Cha Wananchi (CUF) kilitoa maoni kwa kutumia nafasi na vyombo mbali mbali yanayohusu maeneo ambayo yalipaswa kurekebishwa ili kuifanya Sheria hiyo ikidhi malengo ya kuanzishwa mchakato wa kupata Katiba Mpya. Yapo yaliyoingizwa katika Mswada na yapo ambayo hayakuingizwa. Hata hivyo, ni uhalisia usioweza kupingika kwamba Mswada huo ulipitishwa na Bunge na sasa umeshautia saini kuwa Sheria na kuanzia jana imeanza kutumika.

Pamoja na kufikia hatua hiyo, tunaamini yale maeneo muhimu yanayopelekea mjadala kuendelezwa yanaweza kuondolewa wasiwasi na manunguniko kwa
2

kuwa na utekelezaji mzuri unaozingatia misingi ya utawala bora wa vifungu mbali mbali vya sheria hiyo.

Yafuatayo ni maoni na mapendekezo yetu kuhusiana na namna bora ya kutekeleza masharti ya baadhi ya vifungu vya Sheria hiyo:

1. Uteuzi wa Makamishna wa Tume ya Katiba pamoja na Sekretarieti yake Sheria imetoa mamlaka na uwezo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kushauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar kuteua Makamishna na Katibu wa Tume ya Katiba ambayo ndiyo itakayokuwa na majukumu ya kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi na hatimaye kuandaa ripoti pamoja na rasimu ya Katiba Mpya. Tunaamini ni jambo muhimu na la lazima kwamba watu watakaoteuliwa kuwa Makamishna na Katibu katika Tume hiyo wawe ni watu waadilifu, wanaoheshimika na kuaminika mbele ya jamii na wenye ujuzi na uzoefu wa kutosha katika masuala ya Katiba wakiwa na uelewa mpana wa mambo ya Sheria, Siasa, Uchumi na Maendeleo ya Jamii. Tunaamini kuteuliwa watu wa aina hiyo kutaijengea heshima na imani kubwa Tume mbele ya jamii na hivyo kuondoa wasiwasi na hofu zinazojengwa za kutokuwepo kwa nia ya dhati na ya kweli ya kupata Katiba ya kidemokrasia inayotokana na Watanzania wenyewe na ambayo hailengi kuendeleza hali iliyopo (status quo). Kwa msingi na hoja hizo hizo, tunapendekeza wajumbe wa Sekretarieti ya Tume ambao kwa mujibu wa Sheria watateuliwa na Waziri wa Katiba na Sheria wa Jamhuri ya Muungano kwa kushauriana na kukubaliana na Waziri wa Katiba na Sheria wa Zanzibar nao wawe ni watu wenye sifa na vigezo hivyo hivyo tulivyovitaja hapo juu.
3

2. Hadidu za Rejea za Tume ya Katiba Moja kati ya maeneo ambayo yalitolewa maoni na wengi ni haja ya Hadidu za Rejea za Tume ya Katiba kujulikana mapema na kufanywa sehemu ya Sheria hiyo kama Jedwali. Sheria imetoa mamlaka na uwezo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano akishauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar kutayarisha na kutoa Hadidu hizo za Rejea. Sheria yenyewe imetaja baadhi ya kazi za Tume lakini pia ikatamka kwamba Tume itafanya kazi na kutoa mapendekezo yake kwa kila hadidu ya rejea watakayopewa. Wasiwasi uliojengwa ni kwamba Rais anaweza kuibana na kuidhibiti Tume kwa kutoa hadidu zinazobana uwezo na mamlaka ya Tume katika kufanya kazi zake. Tunapendekeza kwamba Hadidu za Rejea zitakazotolewa ziwe zinazotoa uhuru mpana na zisizobana kwa namna yoyote ile Tume au wananchi kutoa maoni kwa maeneo yote watakayoona yanapaswa kuzingatiwa na kuwemo katika Katiba Mpya. Tunapendekeza pia kwamba ili kujenga kuaminiana na kuondoa hofu ya maeneo yepi Tume wamepewa kuyafanyia kazi, basi Rais azitoe hadharani na kuzichapisha katika vyombo mbali mbali vya habari hadidu hizo za rejea. 3. Uhuru mpana usio na vikwazo wa wananchi katika kutoa maoni Ili kuimarisha misingi ya imani kwamba Katiba Mpya itakayoandikwa itatokana na matakwa ya Watanzania na kwamba wao ndiyo watakaoihodhi na kuimiliki, tunaamini Serikali inapaswa iwahakikishie wananchi kwamba watakuwa na uhuru mpana usio na vikwazo katika kutoa maoni yao kwa maeneo yote watakayoona yanafaa kutolewa maoni alimradi tu wanafanya hivyo kwa njia za amani na utulivu. Ni muhimu kuondoa dhana hata ndogo kwamba Serikali ina lengo la kubana uhuru wa wananchi katika zoezi hili muhimu au kwamba ina lengo la kuwafanya watoe mapendekezo yale tu yanayotakiwa na Serikali iliyopo madarakani.

4. Marekebisho ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Sekretarieti yake Hatua ya mwisho ya kuhalalisha Katiba Mpya iliyowekwa kupitia Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, 2011 ni ile ya wananchi kupiga kura ya maoni ya kuikubali au kuikataa Rasimu ya Katiba hiyo. Sheria imetoa mamlaka na uwezo kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, kila moja kwa upande wake, kuendesha na kusimamia kura ya maoni hiyo. Si siri kwamba wadau wengi vikiwemo vyama vya siasa, taasisi na jumuiya za kijamii na kiraia wamepoteza imani na Tume hizo kwamba si Tume huru na adilifu zenye uwezo wa kusimamia chaguzi huru na za za haki. Kura ya maoni ni aina ya uchaguzi, na kura ya maoni ya kupitisha Katiba Mpya ni zoezi muhimu kuliko pengine uchaguzi wowote katika nchi. Kura hiyo ya maoni ndiyo itakayotoa uhalali wa wananchi kuihodhi na kuimiliki Katiba yao na ndiyo maana hata katika Sheria hii, hatua hii imetajwa kuwa Uhalalishaji wa Katiba Inayopendekezwa. Kutokana na hoja hizo, tunapendekeza kwamba ni muhimu na lazima kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kufanyiwa marekebisho kabla ya 2014 kuzifanya kuwa Tume huru na zinazoaminika mbele ya jamii na wadau wote ili wakati zinasimamia na kuendesha kura hiyo ya maoni zisiwe sababu ya kutiliwa mashaka kwa matokeo ya kura hiyo. Kwa mfano, wadau wengi tukiwemo vyama vya siasa haturidhiki na wala hatukubaliani na mfumo wa sasa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuendelea kuwatumia Wakurugenzi wa Halmashauri (DED) na wasaidizi wao kuwa ndiyo Wasimamizi wa Uchaguzi katika Wilaya na Majimbo. Ili hilo lifanyike, patahitajika Katiba iliyopo sasa na Sheria ya Uchaguzi zifanyiwe marekebisho ili kuweka muundo mpya wa Tume ya Uchaguzi na Sekretarieti yake. Tunapendekeza kwamba wakati kazi ya Tume kukusanya maoni ikiwa inaendelea, basi mchakato wa kufanya marekebisho hayo ya Katiba iliyopo sasa na Sheria ya Uchaguzi uanze kwa kushirikisha Serikali na wadau wengine vikiwemo vyama vya siasa na taasisi na jumuiya za kiraia.

MAENEO AMBAYO YANAPASWA KUZINGATIWA KATIKA KUIFANYIA MAREKEBISHO SHERIA YA MABADILIKO YA KATIBA, 2011 ILI KUIFANYA KUWA SHERIA BORA ZAIDI Mheshimiwa Rais, Ukiacha maoni na mapendekezo hayo kuhusiana na utekelezaji wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, 2011, tunakaribisha hatua uliyoitangaza ya kupokea maoni na mapendekezo ya maeneo ambayo wadau mbali mbali wanaona yanapaswa kurefanyiwa marekebisho katika sheria hiyo ili kuifanya kuwa sheria bora zaidi.

Kwa upande wa CUF, tunatoa maoni na mapendekezo yafuatayo:

Kifungu cha 6 (4): Tunapendekeza marekebisho ya kuondoa sharti linalokataza kiongozi wa chama cha siasa wa ngazi ya Taifa, Mkoa au Wilaya kuteuliwa kuwa Mjumbe wa Tume ya Katiba. Tunaamini kwamba Katiba mbali ya kuwa ni waraka wa kisheria lakini pia ni waraka wa kisiasa unaobeba malengo na matarajio ya Taifa. Katika zoezi la kuandika Katiba ni muhimu kuwa na watu wenye uzoefu mkubwa wa masuala ya kisiasa ambao wengine wanaweza kuwa ni viongozi wa vyama vya siasa. Hivyo, tunadhani kuwa sharti hilo liondolewe.

Kifungu cha 9 (2): Tunapendekeza yale maeneo yaliyotajwa kuanzia kijifungu (a) hadi (i) yasiwekewe vikwazo wakati wananchi watakapokuwa wanatoa maoni yao na wawe huru kutoa maoni yote waliyo nayo ambayo itakuwa ni jukumu la Tume kuyaratibu na kuyakusanya.

Kifungu cha 16 (6) (12): Tunapendekeza kwamba Sheria ifanyiwe marekebisho ili kuruhusu makundi mengine ya kijamii (mbali na Tume ya Katiba) kuweza kuandaa makongamano na mikusanyiko itakayojadili rasimu ya Katiba Mpya itakayokuwa imetayarishwa na Tume ya Katiba alimradi tu itajwe kwamba watakaoratibu na kupokea maoni yatakayotokana na makongamano na mikusanyiko hiyo wawe ni Tume ya Katiba.

Kifungu cha 20 (2) (e): Tunapendekeza kwamba wajumbe 116 watakaotokana na makundi, taasisi na jumuiya za kijamii na kiraia wateuliwe na Rais kwa kushauriana na viongozi wa makundi, taasisi na jumuiya husika ili kuwapa uhalali mkubwa zaidi wa kuwakilisha makundi, taasisi na jumuiya hizo na wasiteuliwe na Rais peke yake.

Kifungu cha 32: Tunapendekeza kwamba kiwango cha kura za wananchi za kuhalalisha Katiba Mpya kibadilishwe kutoka zaidi ya asilimia 50 kutoka Tanzania Bara na zaidi ya asilimia 50 kutoka Tanzania Zanzibar na kuwa angalau theluthi mbili ya kura za NDIO kutoka Tanzania Bara na angalau theluthi mbili ya kura za NDIO kutoka Tanzania Zanzibar. Hii itakuwa ni kwenda pamoja (consistency) na kiwango cha kuipitisha kilichowekwa katika Bunge la Katiba (kifungu cha 24(3)). Iwapo kiwango cha theluthi mbili kutoka kila upande kitaonekana ni kikubwa sana, basi tunapendekeza kiwango kiwe angalau asilimia 60 kutoka kila upande. Tunapendekeza hivi tukiamini kwamba ni muhimu kwa Katiba kupata uhalali mkubwa zaidi wa kuungwa mkono na wale wanaokusudiwa kuimiliki na kuihodhi badala ya kuwa zaidi ya nusu tu ya wananchi waliopiga kura. Kwa Sheria ilivyo sasa, iwapo asilimia 50.1 wataunga mkono kutokam kila upande na asilimia 49.9 wakaikataa, bado Katiba inayopendekezwa itachukuliwa kuwa ni halali. Ni maoni yetu kuwa Katiba kama hiyo itakosa uhalali wa kisiasa kwani takriban nusu ya
7

wananchi watakuwa wameikataa. Kinyume chake, kiwango cha theluthi mbili au angalau asilimia 60 kitatoa uhalali mkubwa wa kisiasa.

Kifungu cha 33: Tunapendekeza kifungu kifanyiwe marekebisho ili Tume ya Katiba ivunjwe mara baada ya kukamilisha kazi yake na kukabidhi ripoti na Rasimu ya Katiba Mpya kwa Rais. Tunaona ni kupoteza fedha za walipa kodi bure na kuingia katika gharama zisizo na lazima kwa kuendelea kuibakisha Tume kwa muda mrefu hadi kukamilika kwa kura ya maoni kipindi ambacho haitakuwa na kazi yoyote. Mchakato wa Katiba uliowekwa na Sheria umeweka hatua tatu na vyombo vitatu: Tume ya Katiba: Ukusanyaji wa maoni na kuandikwa kwa Ripoti na Rasimu ya Katiba Mpya. Bunge la Katiba: Kujadili mapendekezo ya Katiba Mpya na kupitisha Katiba. Tume za Uchaguzi: Kuitisha, kusimamia na kuendesha kura za maoni za kuhalalisha Katiba iliyopendekezwa. Tunaona kila hatua ikikamilika, chombo husika kivunjwe na iwapo kutatokea haja ya dharura ya kuitishwa tena, basi Sheria itoe mamlaka hayo kama inavyotoa kwa Bunge la Katiba. Hii itanusuru fedha nyingi za kuendelea kuwalipa Makamishna na Sekretarieti ya Tume wakati wakiwa wamemaliza kazi yao na hawana majukumu mengine. Tunaomba kuwasilisha. HAKI SAWA KWA WOTE

TWAHA TASLIMA MWANASHERIA WA CUF


8

KNY: KATIBU MKUU

You might also like