You are on page 1of 13

MUUNDO WA MUUNGANO NA TAWALA ZA MIKOA Rasimu ya Katiba imependekeza kuendelea kuwa na Muungano wa Tanzania kwa kufanya marekebisho makubwa

ikiwemo kupunguza masuala ya Muungano na kuwepo kwa Serikali 3. Mjadala umekuwa mkali kuhusu Serikali 3 na hata kuzuia mjadala mpana zaidi wa masuala ya muungano. Rasimu haikushughulika kabisa na Serikali ya Tanganyika maana Tume inasema wao walipewa hadidu kuangalia Katiba ya Muungano tu. Kwa hili Tume haikutendea Haki wananchi maana kama wao wamependekeza kuunda Chombo kipya ilikuwa ni lazima kusema chombo hicho kinaundwa namna gani bila kuathiri Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Wakati Mabaraza ya Katiba yanaendelea nchini kote ni vema mjadala wa aina ya utawala kwa Serikali ya Tanganyika na mikoa yake ikapewa fursa pia. Ninaamini kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inapasa kugusia masuala ya msingi ya Katiba ya Serikali ya Zanzibar na Katiba ya Serikali ya Tanganyika. Nina mawazo kadhaa ambayo ningependa yaingie kwenye mjadala wa Katiba mpya.

Muundo wa Muungano

Kwa vyovyote vile muundo unaonekana kukubaliaka na wananchi wengi ni ule wa Muungano wa Serikali 3, Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Tanganyika, japo rasimu imeiita Serikali ya Tanzania Bara. Hata hivyo wananchi wanapoambiwa kuwa kutakuwa na Marais 3, wanaguna. Kwa hiyo suala hapa ni namna gani ya kuhakikisha kuwa tunakuwa na Muundo wa Serikali 3 yenye dola imara na Mamlaka ya Jamhuri yenye nguvu ilhali kila mshirika wa Muungano anakuwa na mamlaka kamili ya kutekeleza wajibu wake kwa Wananchi.

Iwapo tunataka Muungano uwe imara na usitetereke ni lazima tufanye maamuzi ambayo yatabadili sura nzima ya Muungano na kuweka wazi wajibu wa kila Mshirika katika Muungano. Ni vema pia kuweka Muundo wa Serikali ambao utatoa uhuru kwa washirika kutekeleza majukumu yao bila bugudha lakini pia utatoa fursa kwa Dola kutekeleza majukumu yake ya kidola kama kuhakikisha ulinzi, usalama na utulivu wa nchi, kuhakikisha umoja na mshikamano wa nchi na kuhakikisha maendeleo sawia kwa maeneo yote ya Jamhuri ya Muungano.

Napendekeza Muungano wa Serikali mbili za Tanganyika na Zanzibar zinazoongozwa na Mawaziri Wakuu watendaji na Serikali ya Muungano inayoongozwa na Rais. Pia napendekeza masuala ya Tawala za Mikoa kuwa masuala ya Muungano na Wakuu wa Mikoa (Gavana) wachaguliwe na wananchi moja kwa moja na wawe na mamlaka kamili kwenye masuala yatakayokabidhiwa kwa Serikali za Mikoa kwa mujibu wa Sheria itakayotungwa na Bunge la Muungano (Seneti). Napendekeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania achaguliwe na wananchi wote kwa kupata zaidi ya nusu ya kura zote halali na sio chini ya asilimia 25 ya kura kutoka kila upande wa Muungano. Gavana wa Mkoa pia achaguliwe na wananchi wote wa Mkoa husika.

Nafasi nyingine za kuchaguliwa moja kwa moja ziwe ni pamoja na Madiwani ambao watachagua Meya/Mwenyekiti wa Halmashauri, Wabunge wa Mabunge ya Tanganyika na Zanzibar ambapo chama chenye wabunge wengi au muungano wa vyama wenye wabunge wengi utatoa Waziri Mkuu kuongoza Serikali za washirika na Maseneta ambao watachaguliwa na Mikoa kama inavyopendekezwa na rasimu ya Katiba ya sasa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano Napendekeza Rais awe Mkuu wa Nchi, Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama na Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwenye mamlaka kamili kwenye masuala yote ya Muungano yaliyoainishwa na Katiba. Rais wa Jamhuri ya Muungano awe na wajibu wa kikatiba wa kuhakikisha kuwa kuna ulinganifu wa maendeleo kwa mikoa yote ya Jamhuri ya Muungano. Rais awe na Mamlaka ya kukikaribisha chama chenye wingi wa wabunge kwenye mabunge ya Tanganyika na Zanzibar kuunda Serikali. Pale ambapo hakuna chama pekee chenye wingi wa wabunge wa kutosha kuunda Serikali, Rais awe na Mamlaka ya kukipa fursa ya kwanza chama chenye idadi kubwa ya wabunge kujaribu kuunda muungano wa vyama ili kuweza kuunda Serikali. Rais awe na wajibu wa kila mwaka kuongoza kikao cha Mkutano Mkuu wa magavana wa mikoa yote nchini na pia kuhutubia Baraza la Taifa (Seneti, Bunge la Tanganyika, Bunge la Muungano na Mkutano wa Magavana kwa pamoja). Rais atakuwa na mamlaka ya kuthibitisha kuondolewa madarakani kwa Waziri Mkuu kufuatia kura ya kutokuwa na imani iliyopigwa na Bunge

(Baraza la Wawakilishi) la nchi Mshirika au pale Waziri Mkuu anapopoteza uwingi wa viti ndani ya Baraza. Rais atakuwa na mamlaka, kupitia Tume ya Maadili ya Umma, kusimamia maadili ya viongozi wa Umma.

Bunge la Tanzania Kuwe na Bunge la Jamhuri ya Muungano lenye sehemu kuu 2, Bunge la juu (seneti) na Bunge la chini (Bunge la Tanganyika na Bunge la Zanzibar au twaweza kuita Mabaraza ya Wawakilishi). Maseneta wachaguliwe kutoka kila mkoa kwa utaratibu kwamba kila mkoa utatoa maseneta wawili, mwanamke na mwanaume. Kila Bunge la mshirika (Baraza la Wawakilishi) litachagua wananchi 5 ambao sio wajumbe wa Bunge hilo kuwa Maseneta. Wananchi hawa watakuwa wawakilishi wa makundi ya kijamii kama watu wenye ulemavu, vijana na watu wenye ujuzi maalumu. Kila mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano aliyepata zaidi ya asilimia 5 ya kura za Urais atakuwa amechaguliwa kuwa Seneta moja kwa moja. Bunge (Baraza la Wawakilishi) la Washirika wa Muungano

watachaguliwa kwa mujibu wa Sheria zitakazotunngwa na na watatoka kwenye majimbo ambayo ni Halmashauri za Wilaya/Miji/Manispaa/Jiji.

Kila nchi washirika wataweka utaratibu wa kuhakikisha usawa wa kijinsia kulingana na mazingira ya kijiografia ya nchi hizo isipokuwa sio chini ya asilimia 40 ya Wawakilishi watakuwa wanawake.

Waziri Mkuu Atakuwa Mkuu wa Serikali ya nchi mshirika wa Muungano na atakuwa na mamlaka kamili kwa masuala yote yasiyo ya muungano. Waziri Mkuu atatokana na chama chenye Wabunge wengi kwenye Bunge la Nchi mshirika au kama hakuna chama chenye wabunge wengi peke yake kuweza kuunda Serikali, basi atatoka kwenye muungano wa vyama kwa mujibu wa makubaliano ya vyama hivyo na kuthibitishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano. Waziri Mkuu hatokuwa Mbunge na Mawaziri wake hawatakuwa Wabunge isipokuwa uteuzi wao

utathibitishwa na Bunge kupitia Kamati maalumu itakayoundwa na Bunge. Waziri Mkuu pamoja na Serikali yake watawajibika kwa Bunge (Baraza la Wawakilishi). Gavana (Mkuu) wa Mkoa Atakuwa Mkuu wa Serikali ya Mkoa mwenye mamlaka kamili juu ya masuala yote yaliyoidhinishwa kwa mujibu wa Sheria itakayotungwa na

Baraza la Wawakilishi (Bunge). Mkuu wa Mkoa (Gavana) atachaguliwa na wananchi wote wa Mkoa husika na atawajibika kwa BARAZA LA MKOA. Mkuu wa mkoa (gavana) atateua Kamati tendaji wa Mkoa kutokana na Idara zitakazoundwa na Baraza la Mkoa kutokana na Sheria ndogo zitakazotungwa.

Baraza la Mkoa Baraza la Mkoa litaundwa na Wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi/Bunge waliomo kwenye mkoa husika, maseneta wote wa mkoa husika, Mameya na Wenyeviti wa Halmashauri za Wilaya za mkoa husika na madiwani 2, mwanamke na mwanaume, watakaochaguliwa na Baraza la Madiwani la Halmashauri husika. Baraza la Mkoa litakuwa na mamlaka ya kujadili na kupitisha mipango ya maendeleo ya mkoa, kushauri na kusimamia kamati tendaji ya mkoa, kupitisha sheria ndogo za kuendesha mkoa (by laws), kujadili na kuidhinisha Bajeti ya Mkoa na kuthibitisha mikataba yote ambayo mkoa unaingia. Baraza la Mkoa pia litakuwa na wajibu wa kupokea na kujadili na kutoa maelekezo kuhusu taarifa za utendaji za Halmashauri za Wilaya ndani ya mkoa husika.

Mambo ya Muungano Rasimu ya Katiba imeainisha masuala saba ya muungano. Hata hivyo masuala haya hayatoi nguvu ya kikatiba kwa Jamhuri ya Muungano kubakia moja na imara. Masuala kadhaa hayana budi kuongezwa. Usimamizi wa Hifadhi ya jamii (social security) ni suala linahusu uhai wa Taifa na wananchi wake. Pia hifadhi ya jamii ni kama Deni la Taifa (obligation of the State), kwa hiyo ni lazima liwe suala la Muungano. Kila nchi Mshirika anaweza kuwa na Shirika lake la Hifadhi ya Jamii, lakini usimamizi wa Sekta ni vema ufanywe na chombo cha Muungano. Vile vile Usimamizi wa masuala ya Bima na Mabenki kwa sababu haya ni masuala ya sera za fedha. Monetary policy huko tunakokwenda ni suala la monetary Union ya Afrika Mashariki, hivyo suala hili halina budi kuwa suala la Muungano na hakuna mjadala kwenye hilo. Usimamizi na udhibiti wa Sekta ya Nishati (Mafuta na Gesi Asilia na masuala ya Atomiki) yanapaswa kuwa masuala ya Muungano. Kila nchi mshirika anaweza kuwa na kampuni yake ya Taifa ya Mafuta na Gesi lakini masuala ya usimamizi wa sekta ni vema yawe chini ya chombo cha muungano ili kuhakikisha kuwa utajiri wa nchi unanyonywa kwa uendelevu na pia kutoa mamlaka kwa Bunge la Muungano

kupitisha/kuidhinisha mikataba ya kuvuna rasilimali hizo za Mafuta na Gesi. Ni vema pia kuwa na sera moja ya masuala ya atomiki na nyuklia kwa Jamhuri ya Muungano. Rasimu ya Katiba imeondoa suala la usimamizi na udhibiti wa anga kwenye masuala ya Muungano. Nadhani ni vema kuhakikisha kuwa avition, civil and military yanakuwa ni masuala chini ya mamlaka ya Jamhuri ya Muungano. Kila nchi inaweza kuwa na Shirika lake la ndege usafiri wa anga lakini masuala ya usimamizi na udhibiti wa anga yabakie kuwa masuala ya Muungano. Hivi sasa Tanzania nzima inatumia nambari +255 kuitambulisha katika masuala ya mawasiliano ya simu. Rasimu ya Katiba imeondoa suala la mawasiliano ya simu katika orodha ya masuala ya Muungano. Nadhani ni makosa makubwa sana. Suala la usimamizi na udhibiti wa mawasiliano linapaswa kubakia kuwa suala la Muungano na Tanzania nzima ibakie na +255 chini ya mamlaka ya Jamhuri ya Muungano. Rasimu itatupelekea kuwa na code nambari nyingine kwa Tanganyika, nyingine kwa Zanzibar! Masuala ya biashara ya kimataifa na forodha ni masuala yanayoratibiwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki na hivyo haikuwa sawa kuyaondoa kwenye masuala ya Muungano. Kwa mfano, hivi sasa Bunge la Tanzania

au la Uganda au la Burundi hayana mamlaka kabisa kwenye masuala ya forodha maana Bunge la Afrika Mashariki ndio lenye mamlaka hayo na hutunga Sheri ya forodha (Customs Management Act, 2004). Afrika Mashariki ipo kwenye Umoja wa Forodha na kuelekea Soko la Pamoja, hivyo kuondoa forodha na biashara ya kimataifa kwenye masuala ya Muungano ni kutoona mbali. Kama tunataka kujenga Taifa lenye uwiano sawia kielemu ni vema kuoanisha sera za Elimu ya juu angalau. Napendekeza kuwa Elimu ya Juu iwe suala la muungano. Kila nchi washirika inaweza kuwa na vyuo vikuu vyake lakini ni muhimu kuwa na Chuo Kikuu cha Taifa chini ya Serikali ya Muungano. Mikoa inaweza kuanzisha vyuo vikuu vyake isipokuwa SERA ya Elimu ya Juu iwe jambo la Muungano. Usimamizi wa vyo vya ufundi unaweze kuwa chini ya mikoa. Serikali za nchi washirika wanaweza kuwa na sera ya jumla ya elimu na mafunzo ya ufundi.

Mapato Rasimu ya Katiba imependekeza kuwa ushuru wa forodha na mapato kutoka Mashirika ya Muungano ndiwe fedha za muungano. Ninaamini kabisa kwamba Tume ya Katiba haikupata ushauri mzuri kuhusu suala hili. Kwa uzoefu wangu kama Waziri Kivuli wa Fedha, vyanzo hivyo

havitoshi kuendesha DOLA. Dola inapasa kuwa na rasilimali za kutosha na ziada inaweza kugawa kwa washirika na mikoa katika wajibu wa kuhakikisha maendeleo yanawiana. Dola pia inaweza kuwa na miradi ya Muungano. Vile vile, hayo Mashirika ambayo Tume inasema ni yepi maana muungano umependekezewa masuala saba tu. Kuna haja ya kuangalia kwa umakini mkubwa suala hili kama kweli kuna nia ya dhati ya kuendelea kuwa na Muungano.

Mapato ya Muungano 1. Ushuru wa Forodha 2. Mrahaba wa uvunaji wa Rasilimali ambapo 25% itabaki kwenye mkoa wenye rasilimali na 75% itatumika na Serikali ya Muungano kugawa kwenye mikoa kwa mujibu wa formulae

itakayokubaliwa kwa kuzingatia idadi ya watu, kiwango cha umasikini na ukubwa wa kijiografia. 3. Ushuru wa Bidhaa ambapo 60% itagawiwa kwa nchi washirika kwa ajili ya miradi maalumu. 4. Mapato kutoka kwenye kampuni za kibiashara za Serikali ya Muungano na gawio la Benki Kuu ya Tanzania.

Mapato ya Washirika 1. Kodi ya Mapato ya watu binafsi na Makampuni 2. Kodi ya Ongezeko la Thamani au kodi kama hiyo 3. Tozo mbalimbali zitakazotungwa kwa mujibu wa sharia 4. Mapato yasiyo ya kikodi kutoka idara na Wizara za Serikali.

Mapato ya Mikoa 1. 25% ya Mrahaba kutokana na uvunaji wa Rasilimali/maliasili inayopatikana katika mkoa husika 2. 10% ya makusanyo ya kodi ya mapato ya watu binafsi na makampuni kutoka katika mkoa husika 3. Mgawo kutoka Serikali ya Muungano 4. Mgawo kutoka Serikali ya Washirika 5. Tozo mbalimbali zitakazoanzishwa kwa mujibu wa sharia ndogo ndogo.

Deni la Taifa Napendekeza kuwa Deni la Taifa lisimamiwe kikamilifu na Jamhuri ya Muungano. Akaunti ya Deni la Taifa iwe chini ya hazina ya Jamhuri ya Muungano, Jamhuri ya muungano itakopa kwa niaba ya Washirika wa

muungano baada ya mikopo hiyo kuthibitishwa na Baraza la wawakilishi (Bunge ) la nchi mshirika na Seneti. Jamhuri ya Muungano pia itadhamini mikopo ya ndani na ya nje ya Mikoa na Halmashuri za Wilaya.

You might also like