You are on page 1of 4

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA MAWASILIANO, SAYANSI NA TEKNOLOJIA

UANZISHWAJI WA TUME YA TEKNOLOJIA YA HABARI NA MAWASILIANO TAREHE 3 OKTOBA, 2013


Mkurugenzi, Idara ya Habari MAELEZO, Bw. Asah Mwambene; Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari, Bi. Zamaradi Kawawa; Ndugu Wanahabari; Ndugu Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,

Habari za asubuhi. 1. Napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wote mliofika katika mkutano huu muhimu wenye lengo la kuwaelimisha wananchi na wadau wa Sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kuhusu umuhimu wa kuundwa kwa Tume ya kitaifa ya kuratibu, kusimamia na kuendeleza TEHAMA nchini. Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ni moja kati ya Sekta zinazokua kwa kasi hapa nchini na duniani kote na imekuwa ikichangia kikamilifu katika maendeleo ya Taifa na pia imekuwa ikiwezesha sekta nyingine kukua na kuboresha maisha ya wananchi na huduma za jamii kwa ujumla. Kutokana na ukuaji wa Sekta hii, jitihada za makusudi zinahitajika katika kusimamia na kuratibu shughuli za TEHAMA ili nchi iweze kunufaika zaidi kwani mchango wa sekta hii unaweza kuwa mkubwa kama TEHAMA na matumizi yake yataratibiwa, kusimamiwa na kuendelezwa vyema zaidi kuliko hali ilivyo sasa. Katika kuhakikisha masuala ya TEHAMA nchini yanaratibiwa, kusimamiwa na

kuendelezwa vyema, Serikali iliona ni vema ikaundwa Tume ya TEHAMA (ICT Commission). Uamuzi huu pamoja na mambo mengine, unatambuliwa na Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2003 ambayo pia inaelekeza kuundwa kwa chombo cha TEHAMA ikiwemo juhudi na program mbalimbali zinazoendelea hapa nchini zinazohitaji utaratibu wenye ufanisi. Aidha, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia inaendelea na taratibu za uanzishwaji wa Tume ya TEHAMA ikiwepo juhudi na program mbalimbali zinazoendelea hapa nchini zinazohitaji uratibu wenye ufanisi. Kwa kutambua mchango wa wadau katika ukuzaji wa sekta ya Mawasiliano nchini, wadau mbalimbali wa masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wamehusika na kushiriki kikamilifu kutoa maoni katika hatua zote za uanzishwaji wa Tume hii. Tume hii inalenga kutambua na kuvutia fursa za uwekezaji katika TEHAMA, kutoa ushauri, kuendeleza rasilimali watu kitaifa kwenye sekta ya TEHAMA, kuendeleza program za kitaifa za TEHAMA na kushiriki katika kuendeleza miundombinu mbalimbali ya TEHAMA yenye sura ya kitaifa kwa kushirikisha wadau wa sekta zote.

Ndugu Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana,


2. Jitihada za kuanzisha Tume zinalenga kutekeleza Sera ya Taifa ya TEHAMA pamoja na maazimio mbalimbali ya kitaifa na kimataifa ikiwemo maagizo ya Mkutano wa Dunia wa Jamii Habari (World Summit on Information Society). Aidha, jitihada mbalimbali zimefanywa na Serikali katika kuhakikisha Sekta ya TEHAMA inakua nchini. Miongoni mwa jitihada hizo ni pamoja na uanzishwaji wa vituo vya Mawasiliano vya Jamii (community telecentres), ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (National ICT Broadband Backbone-NICTBB), Uanzishwaji wa Wakala wa Serikali Mtandao, Uanzishwaji wa Vituo vya Kutunzia kumbukumbu za TEHAMA (Data centres), na Mradi wa Anwani za Makazi na Simbo za Posta (Physical Adressing System and Postcode).

Ndugu Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana,


3. Mafanikio katika jitihada hizi yamekabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo kutokuwepo kwa chombo mahususi kinachoratibu, kusimamia na kuendeleza TEHAMA nchini. Ni dhahiri kuwa sekta ya Mawasiliano inakuwa kwa kasi kubwa sana duniani kote na hapa nchini kwetu, na hivyo kufanya baadhi ya mambo kuwa na changamoto katika utekelezaji wake hususan kutokuwepo na uratibu wa kitaifa katika miradi na program zenye sura ya kitaifa. Pia, kukosekana kwa mpango wa Kitaifa wa usimamizi wa kuhakikisha kuwa mifumo ya TEHAMA inawasiliana na hatimaye kuepuka upotevu wa rasilimali unaotokana na taasisi mbalimbali kufanya kitu kile kile (duplication of efforts); Changamoto nyingine ni kutokuwapo wataalamu wa na usimamizi, usajili wa kitaifa wa kuendeleza weledi kwa TEHAMA (professional development, registration and

certification) na kuhakikisha utoshelevu wa rasilimali watu utakaokidhi mahitaji ya maendeleo ya TEHAMA; Kutokuwepo chombo mahususi chenye majukumu ya kisheria.

Ndugu Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana,


4. Tume hii inatarajia kuondoa changamoto hizo tajwa hapo juu na kujenga mfumo utakaowezesha uwekezaji wa kushirikisha sekta binafsi katika ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano na TEHAMA yenye sura ya kitaifa; Kuwepo mfumo utakaowezesha wabunifu na wajasiriamali kuendeleza sekta ya TEHAMA; na kuweka utaratibu na miongozo ya namna bora ya kuhifadhi vifaa chakavu vya TEHAMA (e-waste management).

Ndugu Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana,


5. Tume ya Teknolojia, Habari na Mawasiliano itasaidia kukuza uchumi wa Taifa kutokana na kukua kwa sekta ya TEHAMA na kuchochea uzalishaji, ukuaji wa sekta zingine kiuchumi na usambazaji wa huduma za jamii; kuwa na taifa la jamii Habari, lenye wataalam wanaotambulika kitaifa na kimataifa, na wajasiriamali katika Nyanja mbalimbali za TEHAMA kuendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia duniani; kuwa na uhakika wa usalama katika matumizi ya TEHAMA na kuwepo na mfumo unaoainisha na kuendeleza uwekezaji katika sekta ya TEHAMA kitaifa.

Ndugu Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana,


6. Kwa niaba ya Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wadau na wananchi wote wanaoshiriki kwa njia moja au nyingine katika uanzishwaji wa Tume ya TEHAMA nchini.

Asanteni kwa kunisikiliza.


Imetolewa na; Prisca J. Ulomi Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia.

You might also like