You are on page 1of 6

MAHKAMA NDANI YA MIAKA 50 ILIYOPITA ZANZIBAR: MAFANIKIO NA CHANGAMOTO Na ALI UKI, MHADHIRI WA SHERIA, ZANZIBAR UNIVERSITY.

TAREHE: 16 NOVEMBA, 2014 Utangulizi Mahkama imetimiza miaka 50 tokea Mapinduzi ya Januari 12, 1964. Mahkama1, moja katika mihimili mitatu. Katika utekelezaji wa majukumu yake, Mahkama imepita katika vipindi saba tofauti vya uongozi wa nchi ama vimesaidia mafanikio au chachu za changamoto. Vipindi vya uongozi ni kuanzia 1964 mpaka 1972 chini ya uongozi wa marehemu Sheikh Abeid Amani Karume, kutoka 1972 mpaka 1984 chini ya uongozi wa Alhaj Aboud Jumbe, kutoka 1984 mpaka 1985 chini ya uongozi wa Alhaj Ali Hassan Mwinyi, kutoka 1985 mpaka 1990 chini ya uongozi wa marehemu Sheikh Idris Abduwakil, kutoka 1990 mpaka 2000 chini ya uongozi wa Dk. Salmin Amour, kutoka 2000 mpaka sasa 2010 chini ya uongozi wa Mheshimiwa Amani Abeid Karume na 2010 hada sasa chini ya uongozi wa Dk. Ali Mohamed Shein. Vipindi tofauti vya uongozi vimetoa misukumo ya mabadiliko, maendeleo na changamoto za Mahkama. Misukumo iliyotokea ambayo imeleta athari katika utendaji kazi wa Mahkama imesababishwa na mapinduzi fikra za kuendesha mambo wenyewe, misukumo na mageuzi ya siasa, uboreshaji wa sekta ya Mahkama, upanuzi wa siasa za demokrasia na uhuru wa Mahkama. Mkusanyiko huu utasaidia kujenga taswira ya utendaji kazi wa Mahkama na kielelezo kikubwa cha mafanikio ya Mahkama. Michango itakayotolewa itakuwa ni kioo na itasaidia kuimarisha utendaji kazi wa Mahkama na wala haitokuwa chanzo cha chuki cha kutizama sura ya aliyetoa mchango. Baadhi ya Vigezo vya Mafanikio na Changamoto zinazoikabili Mahkama Zanzibar Mafanikio na changamoto za Mahkama Zanzibar zinaweza kutathminiwa katika vigezo tofauti. Baadhi ya vigezo ni hivyi vifuatavyo: (i) (ii) (iii) (iv) (v) (vi) (vii) (viii)
1

Kisheria; Watendaji kazi; Ubora wa maamuzi (seriousness of judgements) yanayotolewa na Mahkama; Uhusiano wa uongozi wa Mahkama na watendaji kazi wa Mahkama; Msukumo wa kisiasa katika utendaji kazi wa Mahkama; Uhuru wa Mahkama; Uelewa wa sheria wa wananchi; Imani ya wananchi kwa Mahkama za Zanzibar;

Kifungu cha 5A (1) cha Katiba ya Zanzibar ya 1984 kinasema kwamba Zanzibar itafuata mfumo wa mgawanyo wa madaraka kati ya mamlaka tatu, Mamlaka ya Utendaji, Mamlaka ya Kutunga Sheria na Kusimamia Utekelezaji wa Shughuli za Umma na Mamlaka ya Kutekeleza Utoaji wa Haki.

(ix) (x) (xi) (xii) (xiii) (xiv) (xv) (xvi) (xvii) (xviii)

Uanzishwaji wa sheria zinazohusiana Mahkama; Uaminifu na maadili ya watendaji wa Mahkama; Virusi vya rushwa dhidi ya baadhi ya watendaji wa Mahkama; Ongezeko la watendaji wa Mahkama (majaji/mahakimu na makadhi); Idadi na aina ya Mahkama; Uteuzi wa watendaji wa Mahkama; Uondoshwaji wa Majaji na mahakimu; Bajeti ya Mahkama; Maslahi ya watendaji wa Mahkama; Urudishwaji wa huduma za mawakili na usajili wa mawakili.

Mafanikio ya Mahkama Zanzibar Baadhi ya mafanikio ni: (1) Mahkama kutokuwa tawi la siasa: Baada ya kuanza mfumo wa vingi mwaka 1992, Mahkama sasa sio tawi la chama cha siasa. Majaji2 na mahakimu hawaruhusiwi kujiunga na vyama vya siasa. (2) Uelewa wa sheria: Kumekuwa na ongezeko la watu kuelewa umuhimu wa sheria na kutumia Mahkama kutatua matatizo yao. (3) Wazawa kushika nyadhifa za jaji na wahakimu: Baada ya Mapinduzi ya 1964, nyadhifa za jaji mkuu, majaji wa Mahkama Kuu na mahakimu zimeshikwa na wazawa badala ya wageni kutoka nje ya nchi. (4) Kuwepo Mahkama Kuu ya Zanzibar: Mahakama Kuu3 imetamkwa katika Katiba ya Zanzibar ya 1984. (5) Kuanzishwa Mahkama za Mahakimu4: Katika kila Wilaya ipo Mahkama ya Wilaya na Mahkama ya Mwanzo. Miaka iliyopitia Mahkama ya Mkoa ilikuwepo Vuga tu . Waliohitaji huduma za Mahkama ya Mkoa walilazimika kusafiri kufika Vuga. (6) Kuanzishwa Mahkama ya Kazi: Ipo Mahkama ya Kazi iliyoanzishwa chini ya Sheria ya Kifungu cha 80 (1) cha Sheria ya Mahusiano ya Kazi Namb. 1 ya 2005. Mahkama hii inasikiliza kesi za migogoro ya kazi. Mahkama hii ni divisheni ya Mahkama Kuu (7) Mahkama ya Kadhi: Mahkama hii imeanzishwa chini ya Sheria Namb. 3 ya 1985. Mahkama hizi zinashughulikia kesi zinazohusiana na ndoa, talaka, mirathi, matunzo ya mtoto.

Kifungu cha 97 cha Katiba ya Zanzibar ya 1984 kinachosema kwamba itakuwa marufuku kwa Jaji wa Mahkama Kuu (pamoja na Jaji Mkuu), Mahakimu wa ngazi zote, Mrasji, Kaimu Mrajisi, Naibu Mrajis na Msaidizi Mrajis na Makadhi wote (pamoja na Kadhi Mkuu) kujiunga na Chama chochote cha Siasa isipokuwa tu kwamba atakuwa na haki ya kupiga kura iliyotajwa katika Kifungu cha 7 cha katiba hii. 3 Kifungu cha 93 (1) cha Katiba ya Zanzibar ya 1984 kinasema kwamba kutakuwa na Mahkama Kuu ya Zanzibar ambayo itakuwa ndio Mahkama ya kumbukumbu na kuwa na mamlaka yote ya kesi za jinai na madai na nguvu nyengine zitazopewa kwa mujibu wa Katiba hii au Sheria nyengine yeyote. 4 Sheria Namb. 6 ya 1985.

(8) Mahkama za Watoto5: Chini ya Sheria hii, Mahkama ya Watoto imeanzishwa na kesi za Mahkama hii zitasikilizwa na Hakimu wa Wilaya kinyume na awali Hakimu wa Mahkama ya Mkoa alipewa uwezo wa kusikiliza kesi zote zinazohusiana na mtoto. (9) Uhuru wa Mahkama6: Katiba ya Zanzibar ya 1984 inatambua uhuru wa Mahkama Zanzibar. (10) Majaji wa Mahkama Kuu kutoondolewa kiholela7. Majaji wamepewa kinga maalum ya kuondoshwa katika nyadhifa zao. Awali Jaji wa Mahkama Kuu angeliweza kuondoshwa kwa mujibu wa utashi wa rais (at the pleasure of the president). (11) Kuanzishwa Sheria ya Mahkama Kuu8 No. 2 ya 1985 (12) Jaji Mkuu kutokuwa Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi ya Mahkama: Baada ya malalamiko, Sheria ya Tume ya Utumishi imefanyiwa marekebisho na Jaji Mkuu sio mwenyekiti wa Tume. (13) Tume ya Utumishi ya Mahkama kutambuliwa katika Katiba9 (14) Ongezeko la majaji: Mahkama Kuu ya Zanzibar ina jumla ya majaji sita wakiwemo majaji wanawake. (15) Kuwepo majaji na mahakimu wanawake: Majaji na mahakimu wanawake wamekuwa sehemu wa watendaji wa Mahkama wanaotoa haki. (16) Ongezeko la Mahakimu: Idadi ya Mahakimu imefikia 63, 47 wapo Unguja na 16 wapo Pemba. (17) Idadi ya Makadhi Imeongezeka: Wapo makadhi 15, 10 wapo Unguja (akiwemo Kadhi Mkuu na Naibu Kadhi Mkuu) na watano wapo Pemba. (18) Maslahi ya majaji na mahakimu kuongezwa: Maslahi ya watendaji hawa yameboreshwa sana kulinganisha na taasisi nyengine. Lakini mahakimu wa Mahkama za Mwanzo wanasikitika. (19) Kuondoshwa Mahkama za wananchi (The Peoples Courts No. 11 of 1969) ambazo zilizokuwa hazifuati mfumo wa sheria ya utoaji haki. (20) Ongezeko la majengo ya Mahkama Unguja na Pemba. (21) Kurejeshwa huduma za mawakili katika Mahkama Zanzibar. (22) Kurejeshwa huduma za mavakil. (23) Idadi ya mawakili walioruhusiwa na Mahkama Zanzibar kuongezeka. Zaidi ya mawakili 100 wamesajiliwa na Mahkama Kuu Zanzibar. (24) Mashirikiano ya Mahkama na asasi za kiserikali na kiraia kuongezeka. (25) Kuanzishwa Siku ya Mahkama (Law Day).

5 6

Sheria Namb. 6 ya 2011. Kifungu cha 5A (3) kinasema kuwa hakuna mamlaka itakyoingilia Mamlaka nyengine isipokuwa na kwa kadri ilivyoelezwa katika Sheria. 7 Kifungu cha 95 (5) cha Katiba ya Zanzibar kinasema kwamba Jaji wa Mahkama Kuu ataondolewa kazini na Rais ikiwa suala la kuondolewa kwake limepelekwa kwa Tume iliyoundwa kwa madhumuni hayo chini ya kijifungu cha (6) cha kijifungu hiki na Tume hiyo imependekeza kwa Rais kwamba Jaji huyo anafaa kuondolewa kutokana kazi zake au kutokana na tabia zake mbaya. 8 Sheria Namb. 2 ya 1985. 9 Kifungu cha 102 cha Katiba ya Zanzibar kinasema kwamba kutakuwa na Tume ya Utumishi ya Mahkama ambayo muundo, kazi na uwezo wake utakuwa kama ilivyoelezwa na Sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi.

Changamoto za Mahkama Zanzibar (1) Rushwa: Tuhuma za harufu ya rushwa kuwepo kwa baadhi ya watoa maamuzi wa Mahkama. Ni vigumu kuithibitisha kwasababu wanaolalamika hawapo tayari kutoa ushahidi. Vile vile, malalamiko yanasikika baada ya kutolewa maamuzi na sio wakati kesi inaendelea. Aidha, kuwepo watu wa kati wa kuunganisha rushwa (middlemen) baina ya baadhi ya watoa haki na wahusika wa kesi/shauri. Rushwa ya Mahkama imegawika mafung yafuatayo: (a) rushwa ya muhali (b) rushwa ya fedha na (c) rushwa ya hisia (perceived corruption). (2) Tuhuma za ushawishi wa wanasiasa kuingilia utendaji kazi wa Mahkama Zanzibar. Inadaiwa kwamba mwenendo na maamuzi ya kesi yanashika (influence) na nguvu za wanasiasa wa ngazi tofauti. (3) Mahkama kuwa masafa marefu na wananchi: Inakuwa vigumu wananchi kwenda mahkamani. Kwa mfano, mkaazi wa Tumbatu au Nungwi inambidi asafiri hadi Mfenesini ikiwa kesi/shauri linalomhusu lipo katika Mahkama ya Mkoa, Mfenesini. Tatizo la masafa linaumiza zaidi kesi inapoingia hatua ya rufaa katika Mahkama ya Mkoa au Mahkama Kuu ya Zanzibar. (4) Majengo ya Mahkama ni mabovu na makongwe: Mfano wa jengo la Mahkama la Makunduchi na Mfenesini. (5) Ukosefu wa nafasi katika majengo ya Mahkama: Kwa mfano, jengo la Mahkama Kuu, Zanzibar lilijengwa mwaka 1908 kukidhi idadi ya wananchi ya wakati huo, lakini halijafanyiwa utanuzi na linafanyiwa mabadiliko ya ndani (internal modification). Baadhi ya Mahakimu hulazimika kutumia chumba kimoja kuendesha kesi tofauti tena kwa wakati mmoja. Jengo la Mahkama ya Wilaya ya Mwanakwerekwe halitoshi na Afisi ya Waendesha Mashtaka ni ndogo mno. (6) Uelewa mdogo wa sheria: Idadi kubwa ya wananchi hawafahamu sheria na baadhi ya wakati wanatarajia Mahkama iamue kwa kufuata matamanio yao. (7) Ukosefu wa Maktaba: Mahkama haina maktaba ya kisasa, ukosefu wa ripoti za sheria na vitabu vya sheria vitakavyowasaidia majaji na mahakimu kuongeza uwezo. (8) Ukosefu wa usafiri kwa Mahakimu: Kinyume na majaji, mahakimu hulazimika kutumia usafiri wa umma na baadhi ya wakati kujikuta wapo pamoja ndani ya gari na ndugu au jamaa ya wahusika kesi jambo ambalo huwatia hofu ua usalama wao. (9) Bajeti ya Mahkama ni finyu: Bajeti ya Serikali imekuwa ndogo na kikomo cha bajeti (ceiling) kinatolewa na Wizara ya Fedha. Aidha fedha zinazoinishwa na Baraza la Wawakilishi zinapatikana kwa asilimia chache. Kwa mfano mwaka wa fedha 2010/2011, jumla ya shilingi 550,000/- za bajeti ya maendeleo ziliidhinishwa lakini zilizopatikana ni shilingi 275,000,000/-, mwaka wa fedha 2012/2013 jumla ya fedha za bajeti ya maendeleo zilizoinishwa na Baraza la Wawakilishi ni shilingi 100,000,000/- lakini zilizopatikana ni asilimia 17 tu ya fedha hizo. Mwaka wa fedha 2013/2014 jumla ya fedha za bajeti ya maendeleo ni shilingi 150,000,000/- lakini hapana uhakika wa kupatikana fedha zote. (10) Mashahidi kutofika mahkamani: Imekuwa tabia baadhi ya mashahidi kutofika mahkamani kutoa ushahidi. Hii inaathiri mno maamuzi ya Mahkama.

(11) Ucheleweshaji wa kesi: Baadhi ya watendaji wa Mahkama wanatuhumiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa kesi kuchelewa kwa visingizio tofauti. (12) Mzigo mkubwa wa kesi kwa mahakimu: Kwa mfano, hakimu wa Mahkama ya Mkoa alikuwa na wastani wa kesi 59 kwa mwaka 2012.10 Hakimu wa Mahkama ya Wilaya alikuwa na wastani wa kesi 178 kwa mwaka 2012.11 Hakimu wa Mahkama ya Mwanzo alikuwa na wastani wa kesi 104 kwa mwaka 2012.12 Wastani wa kesi wa Jaji wa Mahkama Kuu ni 14 kwa mwaka 201213 (13) Utafiti hafifu na uwezo mdogo wa watendaji wa Mahkama. Baadhi ya maamuzi ya Mahkama katika ngazi zote yanaonyesha kukosekana utafiti wa kina wa marudio na uchambuzi makini. Baadhi ya mawakili waliohojiwa walisema kwamba inasikitisha kuona kwamba watendaji wa Mahkama wa ngazi zote wanashindwa kufahamu utaratibu wa mwenendo wa kesi (procedure) na kuathiri haki. Aidha. makadhi wanalalamikiwa kutotumia kitabu au vitabu vya aina moja. Kila kadhi anategemea kitabu anachokipendelea binafsi. Hii inasabisha tofauti ya maamuzi kwa mujibi wa vitabu vya marejeo. (14) Majaji na mahakimu kufunga ushahidi: Baadhi ya wakati, majaji au mahakimu kufunga ushahidi. Jukumu la kufunga ushahidi la la upande wa mashtaka. Athari yake ni kukatwa rufaa, mfano Mahkama ya Rufaa Tanzania lakini maamuzi ni kesi ianze kusikilizwa tena jambo ambalo linaathiri mno upatikanaji wa mashahidi kwa mara ya pili. (15) Mahakimu wapya kutopata mafunzo ya Mahkama: Baadhi ya mahakimu wanaajiriwa moja kwa moja kutoka Chuo Kikuu na bila ya kupata mafunzo wanapewa kesi. Matokeo yake ni ukiukwaji wa utaratibu katika upatikanaji wa haki. Inadaiwa kwamba baadhi ya mahakimu wapya hawajiamini na wanababaika mno anapokuwa wakili mbele yao. (16) Majaji na Mahakimu: Utafiti umeonyesha kwamba baadhi ya mawakili wanalalamika kwamba majaji na mahakimu wanaegemea zaidi upande wa mashtaka katika kuendesha kesi na baadhi ya wakati majaji/mahakimu wanajisahau na kuuliza maswali kama wanawasilisha kesi (make submission,) wanauliza maswali ya kujenga kesi ya upande wa mashtaka dhidi ya walalamikiwa. (17) Majalada ya kesi kufichwa: Utafiti unaonyesha kwamba baadhi ya makarani ama kwa kupewa maelekezo na majaji au mahakimu au wanawasingizia, huficha majalada ya kesi ili kudhoofisha utendaji wa haki. (18) Baadhi ya Majaji na mahakimu kuwachagulia wakili wahusika wa kesi: Ushahidi unaonyesha kwamba watoa haki huwapigia simu mawakili na kuwaelekeza kupokea kesi kutoka kwa mlalamikaji au mlalamikiwa. Kitendo hiki kinadhoofisha haki kutendeka na kuonekana kutendeka. (19) Vitisho dhidi ya wahusika wa kesi: Utafiti unaonyesha kwamba baadhi ya majaji na mahakimu ni wakali sana na hutoa kauli zinazowatisha au kuwakatisha tama wahusika wa kesi.
10 11

Tanzania Human Rights Report, Part II on Zanzibar, 2012, pg 321. Ibid. 12 Ibid, pg. 322. 13 Ibid, pg 321.

(20) Mahudhurio ya majaji na mahakimu kazini: Utafiti unaoyesha kwamba mahudhurio ya waheshimiwa hawa yanalalamikiwa. Wanafika na kuondoka kazini kwa kufuata ratiba binafsi za mambo yao. (21) Kigezo kinachotumiwa na Jaji Mkuu kupanga kesi: Utafiti unaonyesha kwamba Mheshimiwa Jaji Mkuu hana kigezo maalum cha kupanga kesi kwa majaji wa Mahkama Kuu. Baadhi ya wakati, majaji wanalalamikiwa kukataa kupokea kesi bila ya sababu ya msingi ya sheria. (22) Wazee wa Mahkama: Inalalamikiwa kwamba Vifungu vya 239, 240, 242, vya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Namb. 7 ya 2004 hakifuatwi katika kuteua wazee wa Mahkama na wengine hawana uwezo wa kusoma. (23) Uteuzi wa Majaji: Inashauriwa kwamba mawakili wakazingatiwa katika uteuzi wa majaji wa Mahkama Kuu ili kupatikana watendaji wazuri wa kutoa haki. (24) Kuondoshwa kazini mahakimu: Utafiti unaonyesha kwamba baadhi ya mahakimu waliondoshwa kazini kwa visingizio vya siasa. (25) Imani ndogo ya wananchi kwa Mahkama: Utafiti umeonyesha kwamba wananchi wa Zanzibar wana imani ndogo ya uwezo na uadilifu wa baadhi ya watendaji wa Mahkama na wanasikika wakisema kwamba haki itapatikana Mahkama ya Rufaa ya Tanzania na Haki haipatikani Mahkama za Zanzibar (26) Vifaa vya kisasa vya teknolojia katika shughuli za Mahkama. Hitimisho Yaliyoelezwa katika mada hii ni machache kati ya mafanikio na changamoto za Mahkama. Mafanikio na changamoto nyengine zitaelezwa na washiriki. Ni muhimu Mahkama ikawa makini kusikiliza hususan changamoto ili kuzifanyia kazi kwa madhumuni ya kufanikisha utendaji wa haki. Maoni yatakayotolewa na washiriki yasitumike kama daraja la kujenga chuki baina ya washika dau wa sekta ya Sheria. Inawezekana baadhi ya mafanikio na changamoto zimesababishwa na Sheria ziliopo. Uongozi wa Mahkama ujitahidi kuboresha baadhi ya mambo na kushinikiza kuongezwa zaidi bajeti ya Mahkama ambayo imekuwa kikwazo cha utendaji haki hapa Zanzibar.

You might also like