You are on page 1of 3

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

IDARA YA HABARI-MAELEZO

Simu: +255-22-2126826, Mtaa wa Samora,


Baruapepe:maelezo@habari.go.tz, S.L.P 8031,
Tovuti: www.tanzania.go.tz, DAR ES SALAAM.
Faksi: +255-22-2126834.
TAARIFA KWA UMMA

UFAFANUZI KUHUSU PROPAGANDA NA UPOTOSHAJI WA TUNDU LISSU

Dodoma, Julai 18, 2017:

Vyombo mbalimbali vya habari leo vimemnukuu Mbunge wa Singida Mashariki Ndugu
Tundu Lissu ambapo pamoja na mambo mengine, huku wakati fulani akitumia lugha za
kuudhi, uchochezi na kejeli, ameituhumu Serikali kuwa inabana demokrasia nchini.

Tunachukua fursa hii kumshauri Ndugu Tundu Lissu ambaye pia kwa nafasi yake kama
Wakili wa Mahakama Kuu ni Afisa wa Mahakama walau basi atekeleze wajibu wake wa
kusimamia weledi badala ya kila wakati kuyatazama mambo kwa jicho la siasa.

Madai kwamba Serikali inakandamiza demokrasia ni propaganda tu za kisiasa. Hii ni kwa


sababu Ndugu Lissu anaonekana kuchanganya kati ya haki katika demokrasia ambazo hata
yeye amezitumia kuongea na wanahabari bila tashtiti kwa upande mmoja na misingi ya
wajibu kwa upande mwingine ambayo kila mmoja, iwe Tanzania au kwingineko duniani,
anayo na pale anapoikiuka hatua huchukuliwa.

Tofauti na upotoshaji wa Ndugu Lissu, Tanzania ikiwa nchi kiongozi Afrika na duniani
katika kuenzi demokrasia na kupigania haki, si tu inaendelea kuenzi misingi hiyo bali pia
imechukua hatua za wazi kuhakikisha kuwa misingi hiyo inalindwa na pale mtu na hata
taasisi zinapokiuka basi mkondo wa sheria, jambo muhimu katika utawala bora, huchukua
nafasi yake.

Mintaarafu tu, ikiwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa (UN), Tanzania imeridhia Mkataba
wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa mwaka 1966 na huwasilisha taarifa zake za
utekelezaji wa demokrasia na haki za binadamu katika Kamisheni ya UN ya Haki za
Binadamu.

Kikanda, Tanzania ikiwa mwanachama kiongozi wa Umoja wa Afrika (AU) imeridhia pia
Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu na ni miongoni mwa nchi za kwanza
kabisa Afrika kukubali kushtakiwa na wananchi wake kwa kuridhia itifaki ya Mahakama ya
Afrika ya Haki za Binadamu na pia kukubali kufanyiwa ukaguzi katika utawala bora kupitia
Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM).

1
Kitaifa, pamoja na kuruhusu tasisi anuai za umma na binafsi, Serikali ya Tanzania ni
miongoni mwa mataifa machache Afrika yaliyotunga sheria ya ndani ya nchi inayowapa
wananchi wake haki ya kuishitaki Serikali au watu wengine wanapoona wamevunjiwa haki
zao za kidemokrasia au kibinadamu (The Basic Rights and Duties Enforcement Act, 1994).

Katika mawanda ya mikataba ya kimataifa, tofauti na upotoshaji wa Ndugu Lissu, misingi


yote ya uhuru iwe demokrasia, kujieleza na haki nyingine za kibinadamu imewekewa katika
mtindo wa haki na wajibu na mataifa yote, ikiwemo Tanzania na yale anayodhani
yatamsaidia, huchukua hatua madhubuti kulinda haki hizo lakini pale wajibu unapokiukwa
hatua kali huchukuliwa.

Ndio maana tumejiuliza hivi anapotoa mfano wa Bunge kutokuwa live (mbashara) siku
nzima kuwa ni dalili ya demokrasia kubanwa nchini Ndugu Lissu amejiuliza hayo mataifa
anayojaribu kushawishi yaisuse Tanzania ni mangapi katika nchi zao ambako Bunge
huoneshwa mbashara walau kwa takribani saa mbili au zaidi kwa siku kama Tanzania
inavyofanya sasa?

Tumeona pia akikejeli mahakama za nchi. Hivi Ndugu Lissu amejiuliza ni mara ngapi yeye
binafsi au wabunge wenzake wa upinzani wameshinda kesi katika mahakama anazozituhumu
kila siku kuwa haziko huru?

Ni kwa sababu hizi basi tunamuasa Ndugu Lissu na wananchi kwa ujumla kujiepusha na
propaganda, kejeli na uzushi usio na msingi dhidi ya Serikali au taasisi zake na pale ambapo
wanadhani kuna haki zimekiukwa badala ya kuvunja sheria ni vyema kutafuta haki kupitia
mkondo wa kisheria ambao tumeuainisha hapo juu.

Serikali itaendelea kuenzi na kuilinda misingi ya demokrasia, uhuru wa watu na kuwapa fursa
wananchi kushiriki katika uchumi wa nchi hasa wakati huu wa mageuzi makubwa ya
kiutendaji chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli lakini haitavumilia mtu yeyote au kikundi
chochote kitakachojaribu kutumia uhuru wowote vibaya ili tu kukwaza azma hiyo ya Taifa.

Imetolewa na:

Dkt. Hassan Abbasi

Mkurugenzi, Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali.

2
3

You might also like