You are on page 1of 2

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA RAIS
Simu Na: +255 (026) 2963630 Menejimenti ya Utumishi wa Umma
Nukushi: +255 (026) 2963629 na Utawala Bora,
Barua Pepe: ps@utumishi.go.tz Jengo la Taaluma Na. 1,
Tovuti:http://www.utumishi.go.tz Chuo cha Masomo ya Biashara na Sheria,
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM),
Barabara ya Mkalama,
S.L.P. 670,
40404 DODOMA.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

MHE. KAIRUKI AITAKA BODI YA USHAURI YA CHUO CHA UTUMISHI WA UMMA


TANZANIA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAKE KWA KUZINGATIA DHIMA YA
UANZISHWAJI WA CHUO HICHO

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,


Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) ameitaka Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa
Umma Tanzania kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia dhima ya uanzishwaji wa
chuo hicho ili kuwa na Watumishi wa Umma watakaoweza kumudu vyema majukumu
yao.

Mhe. Kairuki amesema hayo leo wakati akizindua Bodi ya Ushauri ya Chuo cha
Utumishi wa Umma Tanzania jijini Dar es Salaam.

Mhe. Kairuki amesema Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kilianzishwa kwa lengo
la kutoa mafunzo kwa Watumishi wa Umma ili kuwawezesha kumudu vyema majukumu
yao na kwenda sambamba na kasi ya mabadiliko katika Utumishi wa Umma pamoja na
kutoa ushauri wa kitaalam na kufanya tafiti tumizi katika nyanja mbalimbali.

Pamoja na kuwa tuko kibiashara, lakini Chuo hiki kilianzishwa kwa lengo la
kuwanufaisha Watumishi wa Umma, hivyo ni vyema Watumishi hawa wakanufaika zaidi
kuliko watu wengine au kuwe na uwiano sawa. Bodi ya Ushauri wa Chuo cha Utumishi
wa Umma Tanzania ina jukumu la kuhakikisha kuwa lengo hili linatekelezwa kwa ufanisi
mkubwa hii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba mafunzo yanayotolewa na tafiti
zinazofanyika zinaendana na ajenda za Serikali ikiwemo hii ya Serikali ya Awamu ya
Tano ya kufikia Uchumi wa Kati ifikapo Mwaka 2025, Mhe. Kairuki amesisitiza.

Aidha, Mhe. Kairuki amesema ili Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kiweze kufikia
malengo yake kwa ufanisi, Bodi hii ina jukumu kubwa la kumshauri Waziri mwenye
dhamana ya Utumishi wa Umma juu ya masuala yote ya Kisera, Kimkakati na
Kimenejimenti kuhusu uendeshaji wa Chuo ili kutekeleza azma ya kuanzishwa kwake
kama ilivyoainishwa katika Hati ya Kuanzisha Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania
ya Mwaka 2000.

Pamoja na majukumu mengine mengi ya Bodi hii, Mhe. Kairuki amewaarifu Wajumbe
hao baadhi ya majukumu machache ambayo ni Kutoa ushauri katika mipango yote ya
maendeleo ya Chuo; Kutoa ushauri kuhusu malengo ya Chuo; Kujadili na kupitisha
Mpango kazi na Bajeti ya Chuo; Kupokea na kujadili taarifa ya Mwaka ya utendaji kazi
na fedha kwa ujumla; na Kufanya tathmini ya Mwaka ya Utendaji wa Chuo pamoja na
masuala mengine muhimu kama yalivyoainishwa katika Hati iliyoanzisha wakala huu.

Majukumu haya ni makubwa na muhimu sana kwa ustawi wa Chuo na sekta nzima ya
Utumishi wa Umma kwa ujumla. Hivyo nina matarajio makubwa kwamba, mtatekeleza
majukumu hayo na mengine ambayo sikuyataja lakini yameelezwa katika Sheria husika
ili kuhakikisha kwamba, Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kinakidhi matarajio ya
wadau na kuleta tija na ufanisi katika Utumishi wa Umma nchini, Mhe. Kairuki
ameongeza.

Naye Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Dkt. Charles Msonde ameishukuru Serikali kwa imani
kubwa iliyonayo hata kuweza kuwateua kushika nafasi hizo.

Sio kwamba sisi tunaweza sana, wapo wanaoweza zaidi yetu, lakini tunakushukuru
Mhe. Waziri kwa kutuamini na kutuona tunafaa kuwa washauri wa Chuo cha Utumishi
wa Umma Tanzania hata kututeua, tunaahidi tutatekeleza majukumu yetu ipasavyo na
kuhakikisha chuo kinakuwa na tija na kufikia malengo.Dkt. Msonde amesema.

Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania inaundwa na Wajumbe sita
ambao ni Dkt. Charles Enock Msonde, Mtendaji Mkuu Baraza la Mitihani la Taifa
(NECTA); - Mwenyekiti, Prof. Bernadeta Killian, Mkuu wa Chuo, Chuo Kikuu Kishiriki
cha Elimu cha Mkwawa; - Mjumbe, Bibi Anna T. Maembe, Katibu Mkuu Mstaafu na
Mjumbe wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi; - Mjumbe, Bw. John Ulanga,
Country Director, Trade East Africa Tanzania, Dar es salaam; Mjumbe, Bw. Solanus
Meinrad Nyimbi, Mtendaji wa Mahakama Kuu, Mahakama ya Tanzania; - Mjumbe na Bi.
Roxana Doscar Kijazi, Mkurugenzi, Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu Ofisi ya Rais,
(Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora); - Mjumbe

IMETOLEWA NA:
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI,
OFISI YA RAIS-MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA.
TAREHE 04 OKTOBA, 2017

You might also like