You are on page 1of 20

1

HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA


MAPINDUZI, MHE. DK. ALI MOHAMED SHEIN, KATIKA KILELE CHA
SHEREHE ZA MAADHIMISHO YA MIAKA 54
YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR, UWANJA WA AMAAN
TAREHE: 12 JANUARI, 2018

Mheshimiwa Dk. John Pombe Joseph Magufuli;


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,

Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan;


Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa;


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,

Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi;


Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar,

Waheshimiwa Marais Wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na


Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,

Waheshimiwa Viongozi Wakuu Wastaafu Mliohudhuria,

Waheshimiwa Mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania


na wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,

Mheshimiwa Job Ndugai;


Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,

Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid;


Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar,

Mheshimiwa Profesa Ibrahim Khamisi Juma,


Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

Mheshimiwa Omar Othman Makungu,


Jaji Mkuu wa Zanzibar;

Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa,

Mheshimiwa Ayoub Mohamed Mahmoud;


Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi,

Waheshimiwa Viongozi mbali mbali wa Serikali na Vyama vya


Siasa Mliohudhuria,

Ndugu Wananchi,

Mabibi na Mabwana,
2

Assalamu Aleikum

Kwa unyenyekevu mkubwa namshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba Mbingu na


Ardhi na vyote viliomo ndani yake, kwa kutujaalia uhai na afya njema na tukaweza
kukusanyika hapa hivi leo, kwa ajili ya kuadhimisha miaka 54 ya Mapinduzi Matukufu
ya Zanzibar, ya tarehe 12 Januari, 1964.

Kwa niaba ya Wananchi wa Zanzibar, natoa shukurani zangu za dhati, kwako


Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, kwa kuungana nasi katika sherehe hizi. Kadhalika, natoa shukurani zangu
za dhati kwa viongozi wote wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, waliopo madarakani na waliostaafu kwa
kuhudhuria kwenu. Vile vile, nawashukuru Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya
Kimataifa, Viongozi wa dini na vyama vya siasa na wananchi wote kwa kuhudhuria
kwa wingi katika sherehe hizi muhimu na adhimu. Ahsanteni sana kwa mahudhurio
yenu.

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,


Leo ni siku muhimu sana katika historia ya wananchi wa Zanzibar, ambapo miaka 54
iliyopita, waliikata minyororo ya utawala wa kisultani na vibaraka vyao. Wananchi
wa Zanzibar, walikataa madhila makubwa ya kutawaliwa waliyotendewa na utawala
wa Kisultani, wakoloni, mabwanyenye na mabepari ya kunyimwa haki zao za msingi
katika kuendesha maisha yao. Walibaguliwa katika kupata huduma za afya, elimu,
fursa za kuitumia ardhi yao, walinyimwa fursa za kazi zenye staha na heshima ya
mwanadamu, walinyimwa makaazi bora, walidhulumiwa mashamba yao na kukosa
nafasi ya kuendesha maisha yao na kadhalika. Kwa lengo la kukabiliana na uonevu
huo, Chama cha Afro-Shirazi kilichoongozwa na Rais wake Marehemu Mzee Abeid
Amani Karume, kilivinjari na kilisimama imara kwa ajili ya kuwakomboa wanyonge
wafanyakazi na wakulima wa Zanzibar.

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,


Leo tunapoadhimisha sherehe za Mapinduzi kwa kutimiza miaka 54, hatuna budi
kuwakumbuka na kuwashukuru wazee wetu waasisi wa Chama cha Afro-Shirazi,
walioongozwa na Rais wake wa Kwanza Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, kwa
3

ushujaa wao wa kuzipigania haki zetu, kuleta usawa na maelewano na kuondosha


kila aina ya pingamizi walizokuwa wakizipata wananchi wa Unguja na Pemba. Leo ni
siku ya kumbukumbu ya ushindi wa wananchi wa Zanzibar na kwamba Mapinduzi
yaliuinua na yaliusimamisha utawala wa wanyonge, wakulima na wafanyakazi;
yaliweka usawa na kuwakabidhi tena wafanyakazi na wakulima wa Zanzibar,
heshima yao na utu wao, katika nchi yao.

Namuomba Mwenyezi Mungu amrehemu Jemadari wa Mapinduzi yetu Matukufu ya


tarehe 12 Januari, 1964, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, pamoja na waasisi
wengine wa Mapinduzi hayo, waliotangulia mbele ya haki, awabariki na awaweke
mahali pema peponi, Amin. Kwa wale waliohai, Mwenyezi Mungu awape umri mrefu
na afya njema. Siku zote tutawakumbuka, tutawaenzi, tutawashukuru na
tutawaombea dua kwa kujitolea kwao muhanga kwa ajili ya kutukomboa. Kutokana
na jitihada zao na mapenzi kwa nchi yao, hivi sasa tupo huru na tutaendelea kuwa
huru wakati wote.

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,


Leo tunafikia kilele cha Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 54 ya Mapinduzi ya tarehe
12 Januari, 1964, tukiwa na furaha kubwa na kusherehekea kwa vifijo na hoi hoi,
kama tulivyojionea wenyewe hapa uwanja wa Amaan. Pamoja na hayo, sherehe hizi
zinatukumbusha umuhimu wa kuendelea kuyalinda, kuyatetea na kuyadumisha
Mapinduzi yetu, kama tulivyofanya katika miaka iliyopita kwa mafanikio makubwa.

Vile vile, tunasherehekea umoja wetu uliotokana na Muungano wa nchi mbili


zilizokuwa huru; Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na
kuzaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 26 Aprili, 1964. Muungano
wetu ulianzishwa kutokana na sera sahihi za vyama viasisi vya TANU na ASP na
sasa CCM pamoja na uongozi bora na thabiti wa waasisi wa nchi yetu Marehemu
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume na
viongozi wa awamu nyengine waliofuata baadae.

Katika kipindi hiki cha miaka 54 ya Mapinduzi, tunasherehekea kuwepo kwa hali ya
amani, umoja na maendeleo makubwa yaliyopatikana. Tuna wajibu mkubwa wa
4

kuuenzi na kuuendeleza umoja na mshikamano wetu, ambao ndio siri kubwa ya


kuendelea kuwepo kwa hali ya amani na utulivu yenye kuimarisha maendeleo yetu.
Nnafarijika sana kuona wananchi wa Zanzibar wameungana na Serikali yao katika
kipindi cha miaka 54, kwa kuyatekeleza malengo ya Mapinduzi yetu na kupatikana
maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Kwa hakika, Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, imeweza kuyatekeleza na kuyaendeleza malengo ya Mapinduzi kwa ufanisi
mkubwa.

Mafanikio yaliyopatikana katika Awamu zote Saba, ni ushahidi ulio wazi


unaodhihirisha kuwa katika miaka 54 iliyopita, tumeweza kufanya mambo mengi kwa
mafanikio na ni haki ya kila mmoja wetu kujivunia mafanikio hayo na kuyaendeleza
kwa manufaa yetu na vizazi vya baadae.

Katika sherehe za mwaka huu, jumla ya miradi ya maendeleo 33 mbali mbali


ilizinduliwa na miradi 15 iliwekewa mawe ya msingi, Unguja na Pemba. Ufunguzi na
uwekaji wa mawe ya msingi ya miradi hio inahusisha Umeme, Masoko, Barabara,
Majengo ya Idara ya Serikali, Vituo vya Afya, Studio ya Televisheni, Skuli, Tamasha
la Biashara na kadhalika.

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,


Katika mwaka huu wa tatu, wa kipindi cha pili 2017/2018, cha Awamu ya Saba,
Serikali imetekeleza vizuri Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2015-2020,
MKUZA III na Dira ya Maendeleo 2020 na kupata mafanikio ya kuridhisha.

Juhudi kubwa zilizochukuliwa na Serikali katika kuimarisha uchumi zimewezesha


kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato. Jumla ya TZS. bilioni 548.571 zilikusanywa
katika mwaka 2017 ikilinganishwa na TZS. bilioni 487.474 zilizokusanywa katika
mwaka 2016. Katika mwaka 2017, mapato yameongezeka kwa TZS bilioni 61.097,
ikilinganishwa na makusanyo ya kipindi cha mwaka 2016, ikiwa ni sawa na ongezeko
la asilimia 12.5. Natoa pongezi kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bodi ya
Mapato Zanzibar (ZRB), kwa juhudi zao katika ukusanyaji wa mapato. Kwa upande
mwengine, Pato la Taifa limeongezeka kutoka thamani ya TZS. bilioni 2,308 mwaka
2015 na kufikia thamani ya TZS. bilioni 2,628 kwa mwaka 2016. Pato hii lilikadiriwa
kufikia TZS. bilioni 2,827, mwaka 2017, kwa bei za soko. Katika jitihada tulizoanza
5

kuzichukua mwaka 2011/2012, hivi sasa, utegemezi wa bajeti yetu kwa mwaka
2017/2018, umefikia asilimia 7.3, ikilinganishwa na asilimia 30.2 katika mwaka
2010/2011. Mafanikio haya tuliyopata ni makubwa na ya kupigiwa mfano.

Kasi ya ukuaji wa uchumi wetu kwa bei halisi, imekua kwa asilimia 7.0 kwa mwaka
2017, ikilinganishwa na asilimia 6.8 kwa mwaka 2016. Aidha, Pato la Mtu Binafsi
nalo limeongezeka na kufikia TZS. 1,806,000 ikilinganishwa na TZS 1,632,000 kwa
mwaka 2015. Kasi ya mfumko wa bei ilifikia asilimia 5.6 katika mwaka 2017 kutoka
asilimia 6.7 mwaka 2016. Lengo letu ni kuimarisha uchumi, kupunguza umasikini na
kuifanya Zanzibar kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi wa kiwango cha kati
ifikapo mwaka 2020.

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,


Katika kipindi cha Januari hadi Septemba, 2017 jumla ya miradi 25 iliyopangwa
kuingiza mtaji wa US$ milioni 276.84 iliidhinishwa na Serikali. Miradi hii
itakapokamilika inategemewa kutoa ajira zisizopungua 915. Katika mwaka 2017,
ujenzi wa mji mpya wa kisasa wa Fumba na Nyamanzi imeendelezwa, kwa lengo la
kuimarisha maisha ya wananchi na kubadilisha taswira ya Zanzibar. Jumla ya
nyumba 170 zimejengwa katika Mradi wa ujenzi wa “Fumba Satellite City” na
nyumba 60 katika Mradi wa “Fumba Town Development”, Nyamanzi.

Kadhalika, mradi wa nyumba za kisasa katika eneo la Mbweni unaotekelezwa na


Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) wa ujenzi wa majengo 18 yenye urefu
wa ghorofa 7 unatarajiwa kukamilika, hivi karibuni. Vile vile, mradi wa ujenzi wa
hoteli ya kisasa ‘Verde’ ya nyota tano, inayojengwa huko Mtoni Unguja ambao
unaotekelezwa na Kampuni ya SS Bakhressa, umekamilika. Hatua inayofuata ni ya
uwekaji wa samani. Mradi huu unatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni.

Uimarishaji wa miji yetu umeendelezwa kupitia mradi mkubwa wa Huduma za Jamii


Mijini (Zanzibar Urban Services Project - ZUSP). Awamu ya kwanza ya Mradi huu,
imeshatekelezwa kwa mkopo wa US$ milioni 38 kutoka Benki ya Dunia ambapo
ulijumuisha ujenzi wa miundombinu mbali mbali, ikiwemo misingi ya maji, uwanja
wa Mnazi Mmoja, majengo, ununuzi wa magari kwa Unguja na Pemba na ujenzi wa
ukuta unaolikinga eneo la Forodhani lisiathiriwe na bahari. Ujenzi wa Awamu ya
6

pili ya mradi huu umeshatayarishwa na Benki ya Dunia imekubali kutoa mkopo wa


US$ milioni 55.

Huduma za jamii zimeimarishwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).


Jumla ya kaya 32,478 zimepatiwa TZS bilioni 4.45 katika utekelezaji wa Mpango wa
Kunusuru Kaya Maskini kupitia TASAF III. Vile vile, TASAF III imetekeleza miradi ya
kutoa ajira za muda kwa kaya 27,044 Unguja na Pemba.

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,


Sekta ya utalii imeendelea kuimarika, ambapo jumla ya watalii 433,116 waliingia
nchini katika mwaka 2017, ikilinganishwa na idadi ya watalii 379,242 walioingia
nchini katika mwaka 2016. Hili ni ongezeko la asilimia 14.2, kwa kipindi cha mwaka
mmoja. Kuongezeka kwa idadi ya watalii wanaoingia nchini, kunaonesha wazi
kwamba lengo la kufikia watalii 500,000 ifikapo mwaka 2020, litafikiwa kabla ya
mwaka huo.

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,


Kwa upande wa biashara, jumla ya bidhaa zenye thamani ya TZS bilioni 145.76,
zilisafirishwa kwenda nje ya nchi, mwaka 2017, ikilinganishwa na bidhaa zenye
thamani ya TZS bilioni 94.94, mwaka 2016. Bidhaa zenye thamani ya TZS bilioni
211.42, ziliingizwa nchini kutoka nje ya nchi, ikilinganishwa na bidhaa zenye thamani
ya TZS bilioni 167.09 zilizoingizwa mwaka 2016. Biashara kati ya Zanzibar na
Tanzania Bara inaendelea vizuri, ambapo bidhaa zenye thamani ya TZS billioni 32.32
zilisafirishwa kwenda Tanzania Bara na bidhaa zenye thamani ya TZS bilioni 184.84,
zilisafirishwa kutoka Tanzania Bara kuja Zanzibar katika kipindi cha Januari hadi
Disemba, 2017.

Juhudi za Serikali za kufufua zao la karafuu zinaendelea kupata mafanikio mazuri.


Hadi kufikia tarehe 5 Januari, 2018, jumla ya tani 8,182.04 za karafuu zenye
thamani ya TZS bilioni 114.17 zilikuwa zimenunuliwa kutoka kwa wakulima, katika
mwaka wa fedha 2017/2018. Kwa upande wa mauzo, katika msimu wa mwaka
2017/2018, Serikali imeshauza jumla ya tani 5,881 zenye thamani ya TZS bilioni
103.49. Uamuzi wa kuwalipa wakulima asilimia 80 ya bei ya soko la dunia
7

unaendelezwa. Mwaka huu ni wa sita mfululizo ambapo Serikali inanunua karafuu


kwa wakulima kwa bei ya TZS. 14,000 kwa kilo moja.

Nawashukuru wakulima wa karafuu kwa kuziuza karafuu zao katika Shirika la ZSTC.
Navipongeza vikosi vya Ulinzi na Usalama na Idara Maalum za SMZ kwa kuyadhibiti
magendo ya karafuu.

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,


Mchango wa sekta ya viwanda, katika Pato la Taifa umefikia TZS. bilioni 487.9 kwa
mwaka 2016, ikilinganishwa na TZS. bilioni 417.0 mwaka 2015. Hili ni ongezeko la
asilimia 17 ikilinganishwa na mwaka 2015. Kadhalika, mchango wa sekta ya
viwanda katika jumla ya Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 18.1 mwaka
2015 hadi asilimia 18.6 mwaka 2016.

Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) imeshaidhinisha ujenzi wa


viwanda vinne, katika eneo la Viwanda Vidogo Vidogo Amani pamoja na Maruhubi.
Viwanda hivyo vinajumuisha, Kiwanda cha Mafuta ya Nazi, Kiwanda cha Mafuta ya
Kupikia pamoja na Kiwanda cha Vipodozi, Kadhalika, ujenzi wa viwanda vitatu vipya
vitakavyojengwa huko Fumba umeshaidhinishwa na ZIPA. Serikali itaendelea na
juhudi za kushajihisha wawekezaji wa ndani na nje, kuja kuwekeza katika sekta ya
viwanda.

Serikali kupitia Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) imeendelea kuchukua hatua za


kudhibiti ubora wa bidhaa mbali mbali zinazotengenezwa au kuingizwa Zanzibar kwa
ajili ya matumizi ya wananchi. Jumla ya viwango 143 vimetangazwa kupitia Gazeti
Rasmi la Serikali na vinatumika. Hadi mwezi Disemba 2017, jumla ya bidhaa 12
zimepatiwa cheti cha matumizi ya alama ya ZBS. Ujenzi wa Ofisi na maabara za
ZBS unaendelea katika eneo la Maruhubi.

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,


Katika kipindi cha miaka 54 ya Mapinduzi tunajivunia kuimarika kwa huduma za
elimu ambapo kabla ya Mapinduzi ya 1964, zilikuwa chache, zikitolewa kwa ubaguzi
na zilikuwa za kulipia.
8

Hivi leo, skuli za msingi zimeongezeka mara saba, skuli za sekondari zimeongezeka
mara 53 na idadi ya wanafunzi wa skuli za Msingi na Sekondari imeongezeka mara
14, kutoka wanafunzi 25,372 mwaka 1963 hadi wanafunzi 378,211 mwaka 2017.
Tatizo walilotutengenezea wakoloni kwamba watoto wa wafanyakazi na wakulima
tusiingie sekondari na kupata elimu ya juu, leo halipo tena. Haya ni mafanikio
makubwa ya kupigiwa mfano.

Katika jitihada ya kuongeza madarasa, mwaka 2017, Serikali ilianza ujenzi wa skuli 9
za ghorofa za sekondari kwa Unguja na Pemba, ambapo ujenzi wake, pamoja na
vituo vya mafunzo ya amali kwa Mkoa wa Kusini Unguja na Mkoa wa Kaskazini
Pemba unaendelea. Aidha, ujenzi wa jengo jipya katika Taasisi ya Karume ya
Sayansi na Teknolojia umefikia asimilia 85.

Pamoja na hatua hizo, Serikali inaendelea kulishughulikia suala la ununuzi wa


madawati yote kwa ajili ya skuli zote za Unguja na Pemba. Kutokana na hatua
maalum tunazozichukua za kukusanya fedha, tunatarajia tatizo la upungufu wa
madawati, litamalizika mwaka huu. Kuanzia mwezi wa Julai, 2018 Serikali itaanza
kutekeleza azma ya kurudisha utaratibu wa kutoa elimu bure katika skuli za
sekondari, ili kutekeleza lengo la Mapinduzi. Kwa hivyo, elimu ya Msingi hadi
Sekondari itatolewa tena, bure, bila ya malipo.Hapatakuwa na mzee hata mmoja
atakaetakiwa kulipa na mzigo wote utabwebwa na Serikali.

Mipango yetu ya elimu imepata mafanikio makubwa ambapo sasa Zanzibar inavyo
Vyuo Vikuu Vitatu vinavyoendeshwa na wataalamu wetu wenyewe. Kiasi cha
wanafunzi 1,800 wa fani mbali mbali wanahitimu kwenye Vyuo Vikuu vya Zanzibar,
kila mwaka. Kwa hivyo, Zanzibar itajitosheleza kwa kuwa na wataalamu wake
wenyewe hivi karibuni.

Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,


Juhudi kubwa na za makusudi zinaendelea kuchukuliwa katika kuziimarisha huduma
za afya. Sera mpya ya Afya ya mwaka 2014 inatekelezwa katika kuwapa wananchi
huduma za afya bila ya malipo kutokana na malengo ya Mapinduzi. Hivi sasa
huduma za afya zinatolewa katika hospitali za Serikali 12, badala ya hospitali 5 na
vituo vya afya 158, badala ya 36 vilivyokuwepo kabla ya Mapinduzi. Vile vile,
9

huduma za afya zinatolewa na hospitali za vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na


Idara Maalum za SMZ, mpango ambao kabla ya Mapinduzi haukuwepo.

Kutokana na upungufu wa madaktari mabingwa, madaktari na wataalamu wengine


wa fani ya afya, Serikali imefanya jitihada maalum za kuwasomesha madaktari na
wataalamu mbali mbali wa sekta ya afya. Hadi mwishoni mwa mwaka 2017, jumla
ya madaktari 46 wanasomea masomo ya Uzamili ya Udaktari bingwa, wanafunzi
340 wanasoma Shahada ya Kwanza ya Udaktari, miongoni mwao, 195 wanasoma
katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA). Kadhalika, wanafunzi 1,416
wanasomea fani mbali mbali za afya katika kiwango cha Shahada na Stashahada
katika vyuo tofauti vya ndani na nje ya nchi.

Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,


Idadi ya madaktari wanaotoa huduma katika hospitali na vituo vya afya, Unguja na
Pemba, imeimarika sana. Hivi sasa, daktari mmoja anatoa huduma kwa watu Elfu
nane mia tano na tisiini na mbili (I:8592),. Kutokana na kuongezeka kwa idadi ya
madaktari na wafanyakazi wa fani mbali mbali, kupanuka kwa huduma za tiba na
kinga na kuongezeka majengo ya kutolea huduma; mafanikio makubwa
yamepatikana. Vifo vya akinamama wanaojifungua vimepungua kutoka
237/100,000 mwaka 2016 mpaka 195/100,000 mwaka 2017. Vifo vya watoto
wachanga, navyo vimepungua kutoka 54/1,000, mwaka 2010/2011 hadi 43/1,000,
mwaka 2016/2017.

Kuhusu UKIMWI, pamoja na mafanikio tuliyoyapata, katika kupambana na


maambukizo mapya ya virusi vya UKIMWI, mipango madhubuti imeandaliwa katika
kukabiliana na maradhi hayo thakili. Kwa hivyo, tatizo la UKIMWI bado lipo, ambapo
inakadiriwa Zanzibar hivi sasa ina watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI, ikiwa ni
asilimia 0.4 ya watu wote wa Zanzibar. Mapambano dhidi ya maambukizo mapya
yanahitaji jitihada za kila mmoja wetu.

Kadhalika, kiwango cha malaria na kasi ya kuenea kwake, kimeendelea kudhibitiwa


na kimeendelea kubaki asilimia 0.4 kwa mwaka 2017.
10

Serikali imekabiliwa na idadi kubwa ya wagonjwa na wazazi wanaohudhuria kwenye


hospital na vituo vya afya kwa ajili ya kupata huduma. Idadi ya wagonjwa
wanaotibiwa na kurudi nyumbani (wagonjwa wa nje) imeongezeka kutoka 533,703
mwaka 2010 na kufikia 705,589 hadi Novemba 2017. Hili ni ongezeko la asilimia
32.21. Wagonjwa wanaolazwa nao wameongezeka, kutoka 51,641 mwaka 2010 hadi
kufikia 68,158 hadi Novemba, 2017. Hili ni ongezeko la asilimia 32.0. Ingawa idadi
ya wagonjwa imekuwa ikiongezeka, lakini bado Serikali inaendelea kutekeleza Sera
ya Matibabu bila ya Malipo katika hospitali za umma hadi leo. Pamoja na kuwa
upo upungufu wa vifaa, nyenzo, dawa na kadhalika, lakini Serikali imeongeza nguvu
zake katika kulishughulikia suala hili.

Kwa mfano, tumepata mafanikio ya kutia moyo katika ununuzi na upatikanaji wa


dawa na vifaa vya utibabu, ambapo katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali
ilitenga jumla ya TZS bilioni 4.9, kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa vya utibabu
na katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imetenga jumla ya TZS bilioni 7.0.
Zaidi ya hayo, katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali itatenga kwenye bajeti ya
Wizara ya Afya, jumla ya TZS bilioni 12.0. Uamuzi huu wa Serikali unatarajiwa
kulipatia ufumbuzi wa uhakika wa tatizo la upatikanaji wa dawa na vifaa vya
utibabu.

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,


Pamoja na jitihada za Serikali inazochukua katika kuimarisha huduma za upatikanaji
wa maji safi na salama, bado mahitaji ya maji ni makubwa. Jumla ya lita za maji
milioni 234.45 zinahitajika kila siku kwa Unguja na Pemba, ambapo uzalishaji kwa
siku ni lita milioni 162.82 sawa na asilimia 67 ya upatikanaji wa maji safi na salama.
Kwa upande wa Mkoa wa Mjini Magharibi upatikanaji wa maji ni asilimia 63, Mkoa
wa Kaskazini Unguja asilimia 48 na Mkoa wa Kusini Unguja asilimia 50. Kwa upande
wa Pemba Mkoa wa Kaskazini asilimia 83 na Kusini asilimia 87.

Katika kutekeleza Mradi wa Maji wa Mkoa wa Mjini Magharibi kutokana na mkopo wa


US$ 23.673 kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), visima 9 vipya
vimeshachimbwa na visima 23 vya zamani vimefanyiwa matengenezo. Mabomba
yenye urefu wa kilomita 68 yatalazwa na ujenzi wa matangi utafanywa. Mradi huu
utatekelezwa na Kampuni ya STECOL ya China na kumalizika mwezi Aprili, 2019.
11

Kumalizika kwa Mradi huu kutaongeza upatikanaji wa maji safi na salama kutoka lita
milioni 67 na kufikia lita milioni 81, sawa na ongezeko la asilimia 20.9.

Kampuni ya CRUCS kutoka India inasimamia mradi wa maji, wenye thamani ya


mkopo wa US$ milioni 92 ikiwa ni mkopo kutoka Benki ya Exim ya India. Kampuni
hiyo, tayari imeanza maandalizi ya mradi huo kwa kufanya upembuzi yakinifu.
Maeneo yatakayofaidika na Mradi huo ni Wilaya ya Magharibi A na B.

Kadhalika, Mradi wa maji unaotekelezwa na Kampuni ya “First Highway Engineering”


ya China kwa ajili ya vijiji vya Mkoa wa Kusini na Kaskazini Unguja, umekamilika
Disemba, 2017.

Kuhusu visima 150 vilivyochimbwa katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba,
kwa msaada wa Serikali ya Ras Al Khaimah, visima 26 tayari vinatoa maji na
yanatumika na visima 14 viliendelea kutayarishwa, katika mwaka 2017.

Katika mwaka 2017, Serikali iliendeleza mazungumzo na Kampuni ya RAK Gas ya


Ras Al Khaimah, kwa madhumuni ya kuanza kazi ya utafiti wa Mafuta na Gesi Asilia.
Awamu ya Kwanza ya utafiti huo ilifanywa mwezi wa Machi, 2017 kwa kutumia
ndege ya Kampuni ya “Bell Geospace Enterprises” ya Uingereza iliokabidhiwa
kuifanya kazi hio. Awamu ya pili ya utafiti huo ilifanywa kuanzia tarehe 27 Oktoba,
2017 na Kampuni ya BGP Explorer ya China. Utafiti huu kwenye awamu ya pili
ulihusika katika miamba iliopo kwenye maeneo ya bahari.

Katika mwaka 2018, Serikali inaendeleza utafiti wa mafuta na gesi kwa kutegemea
taarifa itakayotolewa na wataalamu baada ya utafiti uliofanywa. Serikali itatoa taarifa
rasmi kwa wananchi kuhusu matokeo ya utafiti huu unaofanywa kwa maslahi ya
Zanzibar.

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,


Hivi sasa huduma za umeme zinapatikana katika shehia zote za Unguja na Pemba na
wananchi wananufaika na huduma hizi muhimu. Miundombinu ya huduma hizi
imekamilishwa kwa asilimia 91 na mahitaji ya umeme kwa Unguja na Pemba,
yametekelezwa kwa asilimia 60, kwa kadri wananchi walivyojitokeza kuunga umeme.
12

Kwa mwaka 2016/2017 jumla ya vijiji 76 vimefikishiwa umeme na mwezi wa Julai,


2017 umeme umefikishwa katika Kisiwa cha Fundo na tarehe 6 Januari, 2018
umeme ulizinduliwa rasmi. Mpango wa Serikali ni kuufikisha umeme katika Kisiwa
cha Uvinje hapo 2017/2018, Kokota 2018/2019 na Njau 2019/2020. Hadi sasa
tumeshafikisha umeme jumla ya visiwa saba vya hapa Zanzibar. Kadhalika, Serikali
itaendelea na juhudi zake za kuufikisha umeme kwenye vijiji na vitongoji ambavyo
bado havijapata umeme.

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,


Wananchi wanaendelea kupata fursa nzuri ya kuitumia ardhi kwa ajili ya kuendeleza
maisha yao kwa kilimo, ujenzi wa nyumba bora na kadhalika. Kinyume na wakati wa
ukoloni, ambapo hata kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa nyumba kikitozwa kodi, seuze
kupata ardhi kwa ajili ya kilimo.

Katika mwaka 2017, Serikali iliendelea na utaratibu wa kuwapatia wananchi na


wawekezaji nyaraka za kumiliki haki ya matumizi ya ardhi kwa matumizi mbali mbali,
ambapo hati zipatazo 1,400, zitatolewa hivi karibuni. Aidha, zoezi la uhakiki
lililoanza kutekelezwa, litaendelezwa katika maeneo mbali mbali ya ardhi yakiwemo
ya kilimo, uwekezaji na ujenzi wa makaazi, ili kuona yanatumika ipasavyo.

Katika mwezi wa Disemba 2017, Serikali iliandaa Sera Mpya ya Ardhi ya Zanzibar,
ambayo itaimarisha utawala na usimamizi wa sekta ya ardhi. Kuandaliwa kwa sera
mpya ya ardhi kutapelekea kufanyiwa marekebisho sheria nane za ardhi za Zanzibar.

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,


Kwa kutambua umuhimu wa kilimo; Serikali inaendelea kuwapa wakulima ruzuku ya
asilimia 75 ya pembejeo na huduma za matrekta. Hatua hiyo imepelekea, mavuno
ya mpunga kuongezeka kutoka tani 33,655.06 za mpunga kwa mwaka 2013 hadi
tani 39,000 mwaka 2017.

Katika kuwahudumia wakulima kwa msimu wa mwaka 2017/2018, tani 1,800 za


mbolea, tani 350 za mbegu ya mpunga na lita 15,000 za dawa za kuulia magugu
zimenunuliwa na zitasambazwa kwa wakulima. Aidha, katika kuhakikisha kuwa
huduma za matrekta zinakua za uhakika, serikali imeanzisha Wakala wa Serikali wa
13

Huduma za Matrekta na zana nyengine za kilimo. Mbali na matrekta ya zamani


yaliyopo kwenye kiwanda cha matrekta Mbweni, Serikali imetiliana saini Hati ya
Maelewano (MoU) na Kampuni ya Mahindra Mahindra ya India ya kununua matrekta
100 na matrekta 20 kutoka Kampuni ya Mahindra Mahindra tayari yameagizwa.

Serikali imeziimarisha shughuli za utafiti wa kilimo, katika Taasisi ya Utafiti wa kilimo


Kizimbani. Katika mwaka 2017, Taasisi ya Utatifii wa Kilimo, Kizimbani imefanya tafiti
sita (6), katika zao la muhugo, mpunga, mikarafuu, migomba na kunde. Utafiti huo
umeonesha matokeo mazuri na bado unaendelea.

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,


Juhudi zimefanywa na Serikali katika kuimarisha sekta ya uvuvi. Katika mwaka wa
2017, jumla ya tani 24,000.44 za samaki zenye thamani ya TZS milioni 109.17
zimevuliwa. Katika kushajiisha ufugaji wa samaki, Serikali imeanzisha kituo cha
Kutotolea Vifaranga vya Samaki kilichopo Beit el Raas, kwa kushirikiana na Serikali
ya Japan na FAO chenye uwezo wa kuzalisha vifaranga milioni 10 kwa mwaka. Kituo
hiki kinatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni.

Aidha, Serikali imeanzisha Kampuni ya Uvuvi ya Zanzibar (ZAFICO), kwa mtaji wa


TZS bilioni 7 na imeamua kununua meli mbili za uvuvi kwa kuanzia shughuli hizo,
hivi karibuni.

Ili kuongeza kasi ya ufanisi na kuongeza tija katika kuiendeleza sekta ya mifugo,
hivi karibuni Serikali imeanzisha Taasisi mpya ya Utafiti wa Mifugo. Katika mwaka
wa fedha, 2017/2018, Taasisi hiyo imepatiwa TZS. milioni 500 ambapo imeanza
kufanya tafiti 6 ikiwemo athari za minyoo katika ng’ombe na matumizi ya mwani
kama chakula cha mifugo. Kadhalika, jumla ya vikundi 18 vya wafugaji vimepatiwa
ng’ombe 368 na mbuzi 720 wa maziwa kwa mpango wa kopa ng’ombe lipa ng’ombe.
Vile vile, vijana 60 wamepatiwa elimu ya huduma za mifugo vijijini, ili kuwasaidia
wananchi katika vijiji vyao.

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,


Serikali inaendelea na ujenzi wa miundombinu ya barabara mpya katika maeneo
mbali mbali ya Unguja na Pemba. Ujenzi wa barabara ya Jendele - Cheju - Unguja
14

Ukuu (km. 11.7), kwa kiwango cha lami na bara bara ya Kwarara - Matumaini
zimekamilika na zimezinduliwa rasmi jusi katika sherehe za Mapinduzi. Vile vile,
ujenzi wa Barabara ya Bububu - Mahonda - Mkokotoni (km 31) unatarajiwa kuanza
wakati wowote kuanzia sasa kwa mkopo wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Mjenzi wa barabara hio tayari amekabidhiwa eneo la ujenzi huo.

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,


Ujenzi wa barabara ya Chwale (Madenjani) hadi Mzambarau Takao (km. 5.0) na
barabara ya Mgagadu hadi Kiwani (km 7.6), kwa kiwango cha lami huko Pemba nao
umekamilika na tayarinzimezinduliwa. Vile vile, ujenzi wa barabara ya Ole -
Kengeja, (km. 35) unaendelea vizuri, ambapo kazi ya utiaji lami kutoka Ole hadi
Vitongoji (km. 7) umeshafanyika na jitihada zinaendelea. Kadhalika, Serikali
itazijenga kwa kiwango cha lami barabara mbali mbali za vijijini za Unguja na
Pemba katika mwaka 2018.

Katika kuimarisha usafiri wa baharini na usafirishaji wa mafuta, tarehe 02 Disemba,


2017, Serikali ilitiliana saini na Kampuni ya “Damen Shipyard” kutoka Uholanzi kwa
ajili ya kuanza kutengeneza meli mpya ya mafuta. Meli hiyo itakapomalizika
itachukuwa nafasi ya Meli ya MT Ukombozi. Utengenezaji wa meli hiyo utachukua
miezi 18.

Katika kuimarisha usafiri wa anga, ujenzi wa jengo jipya la abiria linalojengwa


kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, uliosita kwa muda
mrefu kutokana na sababu mbali mbali; utaendelea tena hivi karibuni baada ya
kusawazishwa kwa matatizo yaliyojitokeza na ujenzi utakamilika katika miezi 18
ijayo.

Kuhusu ujenzi wa bandari mpya ya Mpiga Duri, ujenzi wake utaanza baada suala la
mkopo wa ujenzi huo kufanyiwa kazi na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na hatimae kujadiliana na Benki ya
Exim ya China, kuhusu mkopo huo.

Aidha, huduma za bandari ya Malindi zimeimarishwa kwa kununuliwa vifaa vipya vya
kuchukulia na kupimia makontena pamoja na vifaa vya kukagulia mizigo na abiria
15

wanaopita kwenye bandari ya Malindi na Mkoani. Katika mwaka 2017, bandari ya


Malindi ilihudumia jumla ya tani za mizigo mchanganyiko 366,918 na makontena
41,967. Bandari ya Mkoani ilihudumia jumla ya tani 56,849.53 za mizigo
mchanganyiko. Lengo la Serikali ni kuzidi kuimarisha huduma za bandari zetu, ili
kuongeza ufanisi na kuchangia ukuaji wa uchumi wetu.

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,


Katika juhudi za kuwaendeleza vijana na wanawake za kupambana na tatizo la ajira,
juhudi kubwa zimefanywa za kuwawezesha kiuchumi kwa kuwapatia mikopo kupitia
Mfuko wa Uwezeshaji Kiuchumi. Kuanzia mwaka 2014 hadi Disemba 2017, jumla ya
Mikopo 1419 yenye thamani TZS. bilioni 2.5 ilitolewa kwa vijana, wanawake na
vikundi mbali mbali vya ujasiriamali. Katika mwaka 2017 jumla ya mikopo 221 yenye
thamani ya TZS. milioni 569.31 ilitolewa kwa wakopaji 3,149 Unguja na Pemba.
Nafasi za ajira 949 zilitolewa Serikalini na ajira 1,644 zilitolewa kwenye sekta binafsi
katika mwaka 2017.

Kadhalika, Serikali imeimarisha ushiriki wa watu wenye ulemavu katika harakati


mbali mbali za kiuchumi na kijamii. Serikali ilianzisha Mfuko wa Watu wenye
Ulemavu mwaka 2012. Mfuko huu wenye jumla ya TZS. milioni 166 umekusudiwa
kutumika kwa kuwapatia mikopo nafuu Watu wenye Ulemavu kuendesha shughuli
zao za kujiajiri wenyewe. Aidha, Serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha
Sera ya Watu wenye Ulemavu itakayotoa utaratibu mzuri wa kuyashughulikia
masuala yao. Kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo.

Kwa upande wa wastaafu, Serikali imeongeza pensheni kwa viwango mbali mbali.
Vile vile, pensheni jamii iliyoanzishwa na Serikali kwa wazee wote waliofikia umri wa
miaka 70, bila ya kuzingatia kazi walizokuwa wakifanya, imeendelea kutolewa kwa
mafanikio. Jumla ya wazee 27,627 wamelipwa jumla ya TZS bilioni 10.175 tangu
utaratibu huo ulipoanzishwa, mwezi wa Aprili, 2016, ambapo kila mzee analipwa
TZS. 20,000 kwa mwezi.

Kuhusu udhalilishaji wa Wanawake na Watoto, jumla ya kesi 177 za udhalilishaji


zilifunguliwa kupitia Operesheni Maalum iliyoanzishwa na Serikali mwaka 2016. Hivi
sasa kesi 90 zinaendelea kusikilizwa Mahakamani Unguja na Pemba. Mpango wa
16

Miaka Mitano wa Kupambana na Vitendo vya Ukatili na Udhalilishaji dhidi ya


Wanawake na Watoto ulizinduliwa mwezi Julai, 2017. Serikali imejenga vituo vipya
vya mkono kwa mkono katika Hospitali ya Makunduchi na Hospitali ya Micheweni
kwa kushirikiana na “Save the Children Fund”. Wito wangu kwa wananchi,
tuendelee kushirikiana katika vita dhidi ya vitendo hivi vinavyoiaibisha na
vinavyoidhalilisha jamii yetu ambavyo vinafanywa kinyume na maadili yetu na haki
za binadamu.

Katika mwaka 2017, Serikali imeimarisha shughuli za Mahkama katika ngazi mbali
mbali ikiwemo Mahkama ya Ardhi na Mahkama ya Watoto. Hivi sasa kasi ya
usikilizaji wa kesi imeongezeka baada ya Serikali kuongeza idadi ya Majaji na
Mahakimu. Juhudi hizo zitaendelezwa kwa kuyafanyia matengenezo makubwa
majengo ya Mahkama, pamoja na kuanza ujenzi wa jengo jipya la Mahakama Kuu
huko Tunguu. Ujenzi wa Mahkama hio unatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Kwa upande wa Baraza la Wawakilishi, Baraza hilo limeweza kutekeleza majukumu


yake vizuri, ambapo katika kipindi cha Januari hadi Disemba mwaka 2017, lilifanya
mikutano minne ambapo jumla ya miswada 14 ilitungwa kuwa sheria. Vile vile,
Jumla ya maswali 529 ya msingi yaliulizwa na kupatiwa majibu.

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,


Kwa kuzingatia umuhimu wa utumishi bora na nidhamu, Serikali imesimamia
utekelezaji wa Sheria Nam. 2 ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2011, ili kuimarisha
uwajibikaji, uwazi na nidhamu katika taasisi zote za Serikali. Serikali imeongeza kasi
ya kupambana na vitendo vya rushwa na uhujumu wa uchumi. Jumla ya taarifa za
uchunguzi 46 zimewasilishwa katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashataka kati ya
mwaka 2016 na 2017 ambapo katika kipindi hicho tayari mashauri tisa kuhusu
rushwa na uhujumu uchumi yamepelekwa Mahkamani. Ni matarajio yangu kwamba
wananchi wataendelea kushirikiana na Serikali katika mapambano hayo dhidi ya
rushwa.

Katika mwezi wa Aprili, 2017 Serikali ilitimiza ahadi yake, ambapo ilipandisha
mishahara kwa watumishi wa umma katika ngazi mbali mbali, ikiwa ni mara ya nne
tangu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba ilipoingia madarakani
17

mwezi wa Novemba, 2010, tumepandisha mshahara mwaka 2011,2012,2013 na


hatimae mwaka jana tumepandisha tena mara ya nne. Mshahara wa kima cha chini
umeongezwa kwa asilimia 100,kwa watumishi wote wa Umma, sambamba na
kuimarisha maslahi yao mengine. Vile vile, nawapongeza waajiri katika sekta
binafsi, kwa kutekeleza agizo la Serikali la kupandisha mishahara ya kima cha chini
kwa wafanyakazi wao. Serikali itahakikisha maslahi ya wafanyakazi katika sekta ya
umma na sekta binafsi, yanaimarika kwa kadri hali ya uchumi inavyoruhusu.

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,


Katika sekta ya habari, Serikali imeendeleza jitihada za kuliimarisha Shirika la
Utagazaji Zanzibar (ZBC) kwa kuweza kuhama kutoka kwenye mfumo wa Analojia
kwenda mfumo wa Digitali. Hatua hii imeongeza kiwango cha ubora wa matangazo
ya ZBC TV. Aidha, matengenezo makubwa yamefanywa katika studio nne pamoja
na kuziwekea vifaa vipya vya kisasa vinavyoendana na mahitaji ya kidigitali
zilizozinduliwa tarehe 9 Januari, 2018. Jengo la ZBC TV la Karume nalo limefanyiwa
matengenezo makubwa. Kwa upande wa ZBC Redio, Serikali imeanunua vifaa mbali
mbali vipya, kuzifanyia matengenezo studio tatu kwa ajili ya kuimarisha matangazo
yake katika kituo cha Rahaleo na Bungi. Ni matarajio yangu kwamba wafanyakazi
wa ZBC nao watatimiza wajibu wao, ili Shirika hili lipata mafanikio makubwa.

Shirika la Magazeti ya Serikali, ambalo linachapisha Gazeti la Zanzibar Leo,


limetayarishiwa mazingira mazuri kwa ajili ya wafanyakazi wake pamoja na kupatiwa
vifaa vya kisasa na ofisi yenye hadhi ya kufanyia kazi za gazeti hilo. Hivi sasa Shirika
la Magazeti la Serikali kwa kushirikiana na Wakala wa Uchapishaji Zanzibar
wamefanikiwa kuanza kuchapisha Gazeti la Zanzibar Leo hapa hapa Zanzibar.
Aidha, Shirika limefanikiwa kuliweka gazeti hili katika tovuti yake jambo ambalo
limewawezesha watu wengi zaidi kupata fursa ya kulisoma. Nauhimiza uongozi wa
Zanzibar Leo uliendeleze gazeti hili, ili lifikie nafasi yake inayostahiki.

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,


Jitihada za kuimarisha michezo zimeendelezwa kwa dhamira ile ile ya waasisi wa
nchi yetu. Matunda ya jitihada hizo yameanza kujitokeza ambapo Timu yetu ya
Zanzibar Heroes, imeonesha umahiri katika mashindano ya “CECAFA Challenge Cup”
ya mwaka 2017. Kadhalika, timu yetu ya “Zanzibar Sand Heroes” ambao
18

wametuletea ushindi na kikombe katika mashindano ya Mpira wa Ufukweni mwaka


jana. Tunazipongeza kwa dhati timu zote mbili. Ushindi wa Zanzibar Heroes umeipa
heshima Zanzibar katika michezo. Kwa mara nyengine natoa shukurani kwa taasisi
zote za Serikali na watu binafsi waliotoa michango mbali iliyosaidia kuziwezesha timu
zetu kupata mafanikio tuliyoyashuhudia. Serikali itaendelea kuimarisha michezo
kwa kuendeleza vipaji mbali mbali na kujenga miundombinu ya kisasa ya michezo
kwa wakati. Na uwanja wa Mao Tse Tung nao umefikia hatua kubwa ya ujenzi hivi
sasa na utakuwa wa kisasa hapo utakapokamilika.

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,


Maendeleo yetu yanategemea sana kuwepo kwa amani na usalama nchini. Jukumu
la kulinda amani na usalama wa nchi yetu ni letu sote kwa kushirikiana na vyombo
vya ulinzi na usalama. Navipongeza vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama kwa
kuilinda nchi yetu na mipaka yake. Napenda niwahakikishie wananchi na wageni
wanaoitembelea nchi yetu kwamba nchi yetu iko salama na kwamba Serikali zetu
mbili zitaendelea kutekeleza wajibu wao wa kikatiba na kisheria katika kulinda
amani, utulivu na maisha ya wananchi na mali zao.

Natumia fursa hii kutoa pongezi zangu kwa Mheshimiwa Dk. John Pombe Joseph
Magufuli katika jitihada zake za kuiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
watu wake pamoja na kupambana na vitendo vya rushwa, ufisadi, uhujumu wa
uchumi, dawa za kulevya na kuzilinda raslimali za nchi yetu. Sote ni wajibu wetu
tumuunge mkono katika vita hivi kwa kuzingatia kuwa rushwa ni adui mkubwa wa
haki na ni adui wa jitihada zetu za kuleta maendeleo nchini.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya


Muungano wa Tanzania katika kuuendeleza na kuuimarisha Muungano wetu. Vile
vile, tutahakikisha kuwa tunashirikiana katika mambo yasiyokuwa ya Muungano
kama tunavyofanya sasa kwa faida ya pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano ya
Tanzania. Mimi na Dk. John Pombe Joseph Magufuli tunatambua uzito wa dhamana
mliyotupa Watanzania, katika kuhakikisha kuwa Muungano wa Tanzania, unadumu
na unaimarika kwa dhamira ile ile ya viongozi wetu wa Awamu zilizotangulia.
Nakuhakikishieni wananchi nyote, kwamba Serikali zetu mbili, zitaendelea kuchukua
19

hatua, ili nchi yetu iendelee kupiga hatua kubwa zaidi na ibaki kuwa nchi ya amani
na utulivu.

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,


Namalizia hotuba yangu kwa kutoa shukurani zangu tena kwa viongozi wote wa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuungana nasi katika
maadhimisho haya ya Miaka 54 ya Mapinduzi. Nawashukuru viongozi wastaafu,
waheshimiwa mabalozi na wawakilishi wa Jumuiya za Kimataifa na Washirika wetu
wa Maendeleo na wageni wetu wote waliohudhuria. Tunaahidi kuendelea
kushirikiana katika utekelezaji wa shughuli mbali mbali za maendeleo, ili kuongeza
ufanisi.

Natoa shukurani na pongezi kwa viongozi wote wa Serikali ya Mapinduzi na


watumishi wote kwa jitihada zao katika kuwatumikia wananchi kwa moyo wa
uzalendo hadi kuyafikia mafanikio tuliyoyapata. Wito wangu ni kwamba tuongeze
kasi katika kutekeleza wajibu wetu kwa misingi ya haki, uadilifu na utumishi bora na
kuwatumikia wananchi katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili katika
maisha yao.

Natoa shukurani maalumu kwa Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho,


inayoongozwa na Makamo wa Pili wa Rais Mheshimiwa Balozi Seif Ali Idi, kwa
uongozi wake mahiri, ambao umezifanikisha sherehe hizi. Kadhalika, shukrani zangu
nazitoa kwa Makamanda wa vikosi vya ulinzi na usalama vya SMT na SMZ pamoja na
wapiganaji wote walioshiriki katika gwaride na kuzifanikisha shughuli zote za
Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 54 ya Mapinduzi; ambazo zimefana sana. Natoa
pongezi kwa wananchi walioshiriki kwenye maandamano na wafanyakazi wa
vyombo vya habari, kwa kuzitangaza shughuli na sherehe zetu tangu katika hatua za
mwanzo za uzinduzi. Kadhalika, natoa shukurani nyingi kwa wananchi kwa
kuhudhuria kwa wingi hivi leo kwenye kilele cha sherehe hizi. Tuendelee kuiombea
nchi yetu amani, umoja na mshikamano, ili tuzidi kupiga hatua za maendeleo.
Nakutakieni nyote kila la kheri na mrudi nyumbani salama, usalimini.
20

MAPINDUZI DAIMA

MUNGU IBARIKI ZANZIBAR


MUNGU IBARIKI TANZANIA
MUNGU IBARIKI AFRIKA

Ahsanteni kwa kunisikiliza.

You might also like